NIMEIPATA barua, kilio mnacholia,
Hali mmetindikiwa, mwashindwa vitu nunua,
Chai mliyojinywea, yaisha kwa kasi mpya,
Salamu baba na mama, muishiko kijijini:
Nia ya kuwasaidia ninayo,
Ila uwezo kwa leo sinao.
Mvua zimekimbia, mjini kwenda tembea,
Kukavu kumebakia, hadi maji yapotea,
Kuyapata imekua, kazi inayolemea,
Salamu baba na mama, muishiko kijijini:
Nia ya kuwasaidia ninayo,
Ila uwezo kwa leo sinao.
Ardhi wamechukua, mgodi wamefungua,
Ahadi mmejaziwa, kuvuja imebakia,
Dhiki mnatazamia, ndiyo inayofatia,
Salamu baba na mama, muishiko kijijini:
Nia ya kuwasaidia ninayo,
Ila uwezo kwa leo sinao.
Ujinga unachipua, juu na chini wakua,
Hapana wa kuwazia, sembuse ya kuvumbua,
Kijiji kinasinyaa, na vijana wakimbia,
Salamu baba na mama, muishiko kijijini:
Nia ya kuwasaidia ninayo,
Ila uwezo kwa leo sinao.
Bonasi nikiambua, nanyi nitawafikiria,
Kidogo kuwatumia, mbaki mnaugulia,
Pengine kitawafaa, siku zikajasogea,
Salamu baba na mama, muishiko kijijini:
Nia ya kuwasaidia ninayo,
Ila uwezo kwa leo sinao.
Mitumba nimechukua, kisha nawaongezea,
Furushi likishakua, kwa basi nawatumia,
Masembere kuyavua, afadhali kuijua,
Salamu baba na mama, muishiko kijijini:
Nia ya kuwasaidia ninayo,
Ila uwezo kwa leo sinao.
Monday, January 9, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment