Sunday, January 8, 2012

Heri ya mwisho mzuri

HUWA ni kubwa fahari, kuwa na mwisho mzuri,
Kuishi kama fakiri, uzikwe kama tajiri,
Dunia kuwa khabiri, japo ulifanza siri,
Heri ya mwisho mzuri, kuliko mwanzo mzuri!

Akachaye ufahari, na kuacha ukafiri,
Akamwogopa Qahari, kwa kila yake kadiri,
Akaiepuka na shari, ujibari na jeuri,
Heri ya mwisho mzuri, kuliko mwanzo mzuri!

Huiacha alfajiri, uione adhuhuri,
Na masaa hudhihiri, ikatinga alasiri,
Magharibi ukikiri, isha tayari hujiri,
Heri ya mwisho mzuri, kuliko mwanzo mzuri!

Hatua zote mahiri, lazima kutasawari,
Na kuchelea ghururi, ili kuambaa shari,
Masaa yakighairi, uzidi kuona shwari,
Heri ya mwisho mzuri, kuliko mwanzo mzuri!

Huropoka ujibari, wenye tadi na kiburi,
Wakaifanza jeuri, kwa wasichokikariri,
Na ikishuka habari, wote huwa yawaadhiri,
Heri ya mwisho mzuri, kuliko mwanzo mzuri!

Hukufuru wenye heri, manane imedhihiri,
Huritadi jemadari, ukiisha uhodari,
Wakabakia sifuri, mbingu zikatahayari,
Heri ya mwisho mzuri, kuliko mwanzo mzuri!

Hili lipe tafakuri, na usiache kufikiri,
Mengi huja kudhihiri, ukisubiri kaburi,
Shari uione heri, uridhie kusubiri,
Heri ya mwisho mzuri, kuliko mwanzo mzuri!

Tawahidi ikariri, mwishoni ikadhihiri,
Mja mwenye kusubiri, njia njema husafiri,
Na kule anakoabiri, lazima hupata kheri,
Heri ya mwisho mzuri, kuliko mwanzo mzuri!

No comments: