Sunday, January 8, 2012

Hofu saini ya moto

MENGINE tukiamua, motoni tutaingia,
Na hasa kuwaibia, wasio nayo hatia,
Yao ukayachukua, yako ukajifanyia,
Usijeukachagua, motoni kwenda ingia:
Hofu saini ya moto, usijeukaitia!

Muamuzi hujifua, rai akaitegemea,
Na lile lenye kuongoa, ndilo analochagua,
Ila anayepotea, vinginevyo hujitia,
Usijeukachagua, motoni kwenda ingia:
Hofu saini ya moto, usijeukaitia!

Waumini tunajua, mengine twajihadaa,
Hofu yatutanguliya, ukweli tunauambaa,
Hilo ninalikataa, nchi isije umia,
Usijeukachagua, motoni kwenda ingia:
Hofu saini ya moto, usijeukaitia!

Nami ninavyopumua, Mola nitamhofia,
Ukweli kutokimbia,hata likija jambia,
Hii si yangu dunia, hilo nilishagundua,
Usijeukachagua, motoni kwenda ingia:
Hofu saini ya moto, usijeukaitia!

Nani atakulilia, ila wanaoshabikia,
Ivute nyuma hatua, haya ukafikiria,
Kwa wema linaloishia, kuwa jema hubakia,
Usijeukachagua, motoni kwenda ingia:
Hofu saini ya moto, usijeukaitia!

No comments: