Tuesday, January 10, 2012

Yafilisika dunia

LEO wanaozaliwa, hawajui kuongoa,
Kuongoza wafifia, na mikakati yavia,
Ujanja wanatumia, akili zimefubaa,

Wengine wamelaniwa, mabavu wanatumia,
Ndumilakuwili wawa, na wengine kwingilia,
Waidhulumu dunia, twazidi kuchanganyikiwa,
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

Wakubwa walojaliwa, haramu wametumia,
Halali kuibagua, na heri kuyoyomea,
Sasa kilichobakia, ni siasa za hadaa,
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

Walonacho wanatwaa, wasonacho kutumia,
Katika kumi wakiwa, wanane wadhulumiwa,
Mkoloni katwachia,ulaji wa kufukua,
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

Wachache walobaki, wazungukwa na hadaa,
Sifa wakilundukiwa, uongo watauchukua,
Ukweli wakakataa, nje unapotokea,
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

Vioo vimeshapotea, wapi kujiangalia ?
Maji wanayatumia, sura yanayochafua,
Huwa kinachotakiwa, sio kweli na usawa,
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

Madubu waingilia, vitisho kuvitumia,
Wengi wanaohofia, lisofaa huridhia,
Mkuku kuchukuliwa, watu yasiyowafaa,
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

Kaskazini ingawa, wapo tusiowajua,
Kimya wanasimamia, bila sifa kungojea,
Nchi zao zinakua, na amani imejaa,
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

Afrika kuna njaa, hata viongozi pia,
Ovyo wanavibugia, hata na vyao raia,
Kisha wanasingizia, hilo wanalosingizia,
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

Na laana zaingia, unafiki ulokua,
Safi wanayemjua, hutaka kumchafua,
Mdogo akitokea, chini humshindilia,
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

Ni uroho na tamaa, yaitawala dunia,
Ukubwa wakimbiliwa, bila kazi kuijua,
Mangimeza watumiwa, wananchi kuwaibia,
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

Matapeli wamejaa, viongozi waingiwa,
Wakija kushtukia, nchi wameiachia,
Kwa bei iliyokuwa, sawa na sifuri kuwa,
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

Matajiri wakamia, uongozi kuutwa,
Si kwa watu kuwafaa, ila wenyewe kupaa,
Na matanuzi kuvaa, kwa ukubwa kuuchukua,
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

Viongozi wa raia, hakuna alobakia,
Madiba kujiondoa, utupu tumeachiwa,
Uchi sasa tunahaha, hapana penye staha,
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

Vijiji twavikimbia, uchungu ulikojaa,
Na madhila yamejaa, waweweseka raia,
Kama tungewanyanyua, nafuu ingelikua
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

Na Mola twamtania, kwa uongo na hadaa,
Kachoka kuvumilia, na sisi si mashujaa,
Zitapozuka balaa, wapi tutakimbilia?
Yafilisika dunia, hakunao viongozi !

No comments: