Saturday, January 28, 2012

Mkubwa ajifanyaye, kuliko ya wananchi

Wakwibao mamlaka, wao wakayachukua,
Na kisha dhima kushika, watumwa sisi tukawa,
Hao ninawaambia, maadui wanakuwa,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi!
Hudhani watu wajinga!

Wajinga huwadhania, watu wakiitikia,
Uzaini ukajaa, na vyeo kujilimbikia,
Na halafu husanzua, hazina kilichokuwa,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi!
Hudhani watu wajinga!

Katiba tulopokea, hata hili inajua,
Mkubwa anayekuwa, ni mwananchi kutambua,
Sio vingine ikawa, kuzuka maharamia,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi:
Katu usimpe nchi!

Wananchi tumeridhia, wao juu wamekuwa,
Ila hawajatuondoa, sisi chini kutupia,
Na kisha kutufagia, kama taka tulokuwa,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi:
Huuza nchi kwa fisadi!

Nchi huwauzia, fisadi na haramia,
Ndani na nje pia, kila kitu kuchukua,
Raia na wazawa, utumwani kuingia,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi:
Huuza nchi kwa fisadi!

Ni mkubwa Mtanzania, hili tunawaambia,
Kilelleni amekaa, wengine ni waajiriwa,
Waweza kuwatimua, katiba vyema ikikaa,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi:
Hugawa nchi kwa wageni!

Na nchi wataigawa, kwa wageni na adawa,
Rushwa wakaichukua, binafsi kutumia,
Wasijali ya raia, na nchi kuitetea,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi:
Hugawa nchi kwa wageni!

Enzi za kujipalia, majivu nayo mkaa,
Kila kitu kukitwaa, hata visivyostahilia,
Mwisho zimeshafikia, upya tutaangalia,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi:
Hulipa wengine tone!

Hulipwa wanaosinzia, sio macho walokuwa,
Nchi wanaoinua, huwa ndio vibarua,
Na nchi wanaoua, sultani wanakuwa,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi:
Hulipa wengine tone!

Pulizo hujifutua, upepo ndani kujaa,
Fahari kujisikia, asichochuma kuliwa,
Matanuzi kutanua, hata yasiyomfaa,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi:
Kazi kwake matanuzi!

Hunyonya waliokuwa, vijijini wanakaa,
Dhuluma kuitumia, maeneo kusinyaa,
Huduma kuwaambaa, hata za msingi zikiwa,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi:
Vijiji huvidharau!

Ni mtu wa kujisikia, hatowatii raia,
Ni watumwa hudhania, kama enzi awalia,
Kutawala ni kugawa, na wananchi kuwaua,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi:
Hujenga makundi nchini!

Ahadi atazitoa, kweli zisizotimia,
Wanachi wakaendelea, kila hali kuumia,
Huku akifurahia, kisicho faa furahiwa,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi:
Huwachuuza raia!

Nchi kwa nje hung'aa, huku ndani inafubaa,
Raia hudhulumiwa, wanyonge waliokuwa,
Pasiwe wa kuwatetea, maisha wakadidimia,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi:
Huwa mbabaishaji!

Swahaba waliokuwa, Omari namfikiria,
Laiti tungejaliwa, na mfano nao tukawa,
Ingepaa Tanzania, wakawa huru raia,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi:
Kazi huwa haiwezi!

Ni nuksi na balaa, hili yafaa kujua,
Ibada na nyingi dua, lazima kushikilia,
Zahama ikapungua, watu tuweze pumua,
Mkubwa ajifanyaye, kuliko yao wananchi:
Ataileta balaa!

No comments: