Saturday, January 28, 2012

Muua demokrasia

Anayefanya bidhaa, raia wa Tanzania,
Wanachama kununua, badala kujijengea,
Heshima ameishiwa, na utu umepungua,
Muua demokrasia, ni adui wa wananchi:
Mjinga ukimpa nchi!



Usimuonee haya, ukweli ni kumwambia,
Chake ukishachukua, kisha ukakitumia,
Na mwingine kuchagua, utu anaoujua,
Muua demokrasia, ni adui wa wananchi:
Wazimu ampaye nchi!

Ni bahau nakwambai, fedha imemuingia,
Ya ufisadi kujaa, na kichwani kuhamia,
Hana la kukufanyia, zaidi ya kukutumia,
Muua demokrasia, ni adui wa wananchi:
Kichaa ukimpa nchi!

Adawa demokrasia, sio wa kuaminiwa,
Mazuri hajakutakia, utumwa atakutiya,
Kisha akang'ang'ania, juu apate kukaa,
Muua demokrasia, ni adui wa wananchi:
Huona wote wajinga!

Watakiwa mhofia, ni mkoma keshakua,
Atakuambukizia, mbali nayeye kimbia,
Salama ubaki kuwa, kwa siha nayo afya,
Muua demokrasia, ni adui wa wananchi:
Mjinga ukimpa nchi!

Akili akuchezaya, na wanaomtumia,
Bei yako kuijua, apate kujiuzia,
Faida akapatia, kwake kubwa ilokuwa,
Muua demokrasia, ni adui wa wananchi:
Wazimu ampaye nchi!

Demokrasia ua, linapaswa kuchanua,
Madhila kuyaondoa, ukubwa wanaojitia,
Kisha kutusanzulia, tukabakia wakiwa,
Muua demokrasia, ni adui wa wananchi:
Kichaa ukimpa nchi!

Amkeni Watanzania, kataeni kutumiwa,
Wengine kunenepea, bungeni wakasinzia,
Hali nyie mwafa njaa, hakuna wa kuwasaidia,
Muua demokrasia, ni adui wa wananchi:
Huona wote wajinga!

No comments: