Saturday, January 21, 2012

Udhalilishaji maiti

Kuna dhifa mwazijua, hakuna asiyeingia,
Kama choo kuingia, hata mkubwa akiwa,
Na chakula kinaliwa, na hai wanaokua,
Udhalilishaji maiti, wote twajidhalilisha!

Na ng'ambo mnapokwenda, tembeleeni mochwari,
Ili mpate jifunda, ujenzi ulio kheri,
Mkirudi kuyatenda, aibu yanayoghairi,
Udhalilishaji maiti, wote twajidhalilisha!

Mwageuka mijipoda, hamuishi kuosheka,
Hamna mnaloganda, akilini kukalika,
Ndio twakosa kuwanda, sasa yayumkinika,
Udhalilishaji maiti, wote twajidhalilisha!

Chumba hiki maalumu, sote lazima kutua,
Mmezishika hatamu, mwashinda kulitambua,
Ufu tambiko muhimu, na staha yatakiwa,
Udhalilishaji maiti, wote twajidhalilisha!

Marehemu kwangalia, wazima hubarikiwa,
Humpendeza alokuwa, juu akiangalia,
Na daraja hunyanyua, kwa ya kesho kuelewa,
Udhalilishaji maiti, wote twajidhalilisha!

Suti leo mwazivaa, chuenlai mlokuwa,
Ila mmezidi fubaa, na utu kupungukiwa,
Wenyewe mwajiangalia, na siyo jumuiya?
Udhalilishaji maiti, wote twajidhalilisha!

Dhahabu ndoo ikiwa, mochwari zaweza jaa,
Nchini zikaenea, hadi vijijini pia,
Ila kinachotokea, maiti twawatania,
Udhalilishaji maiti, wote twajidhalilisha!

Cheichei Tanzania, na nyinyi Watanzania,
Hivi mmeshaambiwa, mochwari hamtaingia?
Nje sinema zatoa, fahari kujivunia,
Udhalilishaji maiti, wote twajidhalilisha!

Zetu ukiziangalia, hutamani kukimbia,
Maiti chini wajaa, na ovyo kufunuliwa,
Laana kubwa sikia, hili ninawaambia,
Udhalilishaji maiti, wote twajidhalilisha!

Fedha tunazitumia, kule kusikotufaa,
Thawabu twazikimbia, jua juu limekuwa,
Machweo yakiingia, jangwani tukaishia,
Udhalilishaji maiti, wote twajidhalilisha!

Makaburi tumeweza, angalau kuwekeza,
Sasa ni kuendeleza, na matunzo kuongeza,
Walotangulia kwanza, haya yatawapendeza,
Udhalilishaji maiti, wote twajidhalilisha!

Rabana tupe jamala, kurehemu walokuwa,
Kitaifa ni suala, lataka walokwishakua,
Wanaojua risala, na amri zilokuwa,
Udhalilishaji maiti, wote twajidhalilisha!

No comments: