Saturday, January 7, 2012

Pambano kuu

Hii mechi ya kushinda, gozi halina makuu,
Mpira budi kudunda, kati, chini pia juu,
Hakuna wa kujipenda, kwa bibi na wajukuu,
Tumbo pambano kuu, twapaswa wote kushinda!

Hapatakiwi vinanda, na hadithi za mafuu,
Watu wataka vibanda, mafiga na matanuu,
Kisha unga kuukanda, chakula kiwe suluhu,
Tumbo pambano kuu, twapaswa wote kushinda!

Kushindwa tunakuponda, ma'na watu si vifuu,
Kwani ni pete na chanda, chakula na kitunguu,
Hapana pa kwenda randa, tumbo ukishadharau,
Tumbo pambano kuu, twapaswa wote kushinda!

Msione twawadanda, chakula sio nafuu,
Watu wakaza mikanda, viuno vyawa mabuu,
Hali zashindwa kuwanda, siasa zatusahau,
Tumbo pambano kuu, twapaswa wote kushinda!

Kama kuna kuwaganda, ni waletao nafuu,
Watupatie matunda, kutulia angalau,
Njaa ije kusarenda, tukasome majuzuu,
Tumbo pambano kuu, twapaswa wote kushinda!

Hili hakuna kupinda, walal halina nahau,
Pambano ili kushinda, chakula kisiwe juu,
Legeza kama mlenda, mateso kuyasahau,
Tumbo pambano kuu, twapaswa wote kushinda!

No comments: