Thursday, January 12, 2012

Mama wa Ujerumani

NI Angela Merkel, meneja twakusifia,
Kiongozi wa ukweli, Ujerumani yapaa,
Kajaliwa mwanamali, meli nahodha afaa,
Mama wa Ujerumani, astahili kusifiwa!

Jerumani marijali, waume wa kutegemea,
Historia bahili, wanawake juu kuwa,
Ila yeye Merkel, kikwazo kakiondoa,
Mama wa Ujerumani, astahili kusifiwa!

Themanini ya ukweli, milioni walokua,
Wamtii mwanamwali, usukani kachukua,
Naye anafanya kweli, nchi yazidi sogea,
Mama wa Ujerumani, astahili kusifiwa!

Kamjalia Jalali, wengine asaidia,
Kazitumia akili, shida zao kuzijua,
Mkakati kajadili, Ugiriki kuokoa,
Mama wa Ujerumani, astahili kusifiwa!

Euro ni mhimili, Ujerumani wajua,
Umoja kuwa kandili, Ulaya bora ikawa,
Na kuzifanya amali, za kuijali dunia,
Mama wa Ujerumani, astahili kusifiwa!

Uingereza kalili, ruia yawapotea,
Hawazioni dalili, inakokwenda dunia,
Wajitia uhalali, kumbe waja kudidimia,
Mama wa Ujerumani, astahili kusifiwa!

No comments: