Sunday, January 29, 2012

Wakataa ukewenza, utaitwa mumesina !

Mariamu sikiliza, ushauri nakwambia,
Usijefanya kuiza, ukaja kuyajutia,
Mkataa ukewenza, sinamume hujakua,
Wakataa ukewenza, utaitwa mumesina !

Amri inaeleza, weye unaitania,
Mwenyewe wajimaliza, kesho kujiharibia,
Dini unaipuuza, kwa kukosa zingatia,
Wakataa ukewenza, utaitwa mumesina !

Ndoa hukupa makazi, kwa wazazi unakaa?
Ndoa hukupa malezi, mumeo kukuangalia,
Ndoa hukupa malazzi, libasi ukaijua,
Wakataa ukewenza, utaitwa mumesina !

Ndoa hukupa malazzi, libasi ukaijua,
Mwenzio kuwa pumzi, nawewe ukapumua,
Kitulizo chenye enzi, kila mmoja akawa,
Wakataa ukewenza, utaitwa mumesina !

Mola ukimkabidhi, moyoni yaliyokuwa,
Hakika huyahifadhi, nawewe ukajaliwa,
Akakupa wema wenzi, ndoa mkawa wabia,
Wakataa ukewenza, utaitwa mumesina !

Atakupa wema wenzi, ndoa mkawa wabia,
Mkawa wasaidizi, nyumba kuiangalia,
Mkapewa na uzazi, udugu mkachangia,
Wakataa ukewenza, utaitwa mumesina !

Na yakiwepo maradhi, wote kujihudumia,
Mkazigawa na kazi, na zamu kujipangia,
Pasiwe na kizuizi, kwa feli kuziamua,
Wakataa ukewenza, utaitwa mumesina !

Ni chuo chenye ujuzi, mengi mtakujayajua,
Na pawapo yake radhi, Mola huyaafikia,
Mkaipanda ngazi, wote peponi kwingia,
Wakataa ukewenza, utaitwa mumesina !


Januari 29, 2012
Dar es Salaam

No comments: