Sunday, January 8, 2012

Wasiojaribu mapya

VIONGOZI walovia, na wananchi kufubaa,
Mapya wasionuia, yakabaki mazoea,
Hivi lini huamgua, ktu waje kuvumbua?
Wasiojaribu mapya, waweza kuendelea?

Wasomi waliokua, shahada wamezivua,
Ila wanagemea, vitu vya kuagizia,
Hawana wanalotoa, raia likawafaa,
Wasiojaribu mapya, waweza kuendelea?

Pampu tunazinunua, hakuna ya Tanzania,
Jenereta nazo pia, Uchina zinatokea,
Kila ukiangalia, ya kwetu haijakua,
Wasiojaribu mapya, waweza kuendelea?

Pasi tunazotumia, nje zote zatokea,
Aidha sindano pia, na vibiriti twajua,
Hili latia kinyaa, vipi tutaendelea,
Wasiojaribu mapya, waweza kuendelea?

Gavana anayajua, ashindwa kuyaongea,
Mfumuko kujatua, kuzalisha yatakiwa,
Maajabu yatakuwa, kwa vitu kuagizia!
Wasiojaribu mapya, waweza kuendelea?

Siasa zetu umbeya, ukweli twaukataa,
Uongo ndio twazua,na ujinga kuulea,
Nchi inadidimia, wajanja twajidhania,
Wasiojaribu mapya, waweza kuendelea?

Nchi isofikiria, yake kujiandalia,
Ikajajitengenezea, watu wanavyovitumia,
Haiwezi endelea, hata karne ikiwa,
Wasiojaribu mapya, waweza kuendelea?

Programu zatakiwa, nchi kuzizingatia,
Kila moja kuinua, chini kilichobakia,
Hadi juu navyo kua, na watu nao kupaa,
Wasiojaribu mapya, waweza kuendelea?

No comments: