Thursday, January 12, 2012

Ni wanachama wetu tu

Viongozi wa kupewa, mara nyingi hubomoa,
Ndio kisa kulilia, watu hawa kuchagua,
Waiongoze mikoa, si kwa cheo ila ridhaa,
Ni wanachama wetu tu, vyeo vinavyowafaa!

Ukiritimba tabia, na ni yetu mazoea,
Kila kitu hukitwaa, hata tusishokijua,
Kura tukishazipewa, lolote hujifanyia,
Ni wanachama wetu tu, ufalme wanajua!

Weupe tulikataa, weusi umeingia,
Yaleyale yalokua, bado yanaendelea,
Hamuwezi kuchagua, tunajua kuchagua,
Ni wanachama wetu tu, ukubwa wanaoweza!

Sammy awaongopea, huku mwenda kupotea,
Hao wamezidi njaa, hawawezi kuongoa,
Yafaa tuliokuwa, kuzidi kuendelea,
Ni wanachama wetu tu, kuongoza watakiwa.

Kula tumeruhusiwa, kwa uhuru kuwaletea,
Shukrani mwatakiwa, hapa kwetu kuzitoa,
Na utumwa kuridhia, mabwana kututambua,
Ni wanachama wetu tu, usultani wajua!

No comments: