Tuesday, January 17, 2012

Mizigo tunayobeba

IBRA kusaidia, mizigo tunayobeba,
Jamala ukishatoa, panda jengine jaruba,
Hata nao wa kuzaa, waweza fata mraba,
Mizigo tunayobeba, ibra kukusaidia !

Chukua vya kuchukua, bali tija si nasaba,
Wajibu watu kufaa, ndugu pia na swahiba,
Lakini haitokuwa, ni yako kesho akiba,
Mizigo tunayobeba, ibra kukusaidia !

Nii uchafu wa kutoa, pamwe kukoga janaba,
Ili kutolaumiwa, dhahabu ikiwa shaba,
Sahani sio sinia, sembuse kuwa kiroba?
Mizigo tunayobeba, ibra kukusaidia !

Mtoa si mpungukiwa, isihesabu vibaba,
Na mitihani ni njia, huweza fika Kaaba,
Yeye akisharidhia, hakuna wa kukukaba,
Mizigo tunayobeba, ibra kukusaidia !

Nani wa kumtegemea, kuliko yeye HIsaba,
Mrabaha aujua, tena hanayo ghiliba,
Kwani akishaamua, chako chote utabeba,
Mizigo tunayobeba, ibra kukusaidia !

Kwako kinachokufaa, utafute ukuruba,
Kwa ibada nazo dua, na vingine vya mahaba,
Naye hujapendezewa, akakutunza hiba,
Mizigo tunayobeba, ibra kukusaidia !

Sahani naiondoa, ijapo haujashiba,
Nenda wengine kugea, njaa iliyowakaba,
Wewe nikikurudia, kilichobaki kubeba,
Mizigo tunayobeba, ibra kukusaidia !

No comments: