Saturday, January 28, 2012

Hasira macho haina

Hasira kweli hasara, yafaa kuipuuza,
Huyu mkubwa kinara, kwa balaa kuongeza,
Kwako iwe ni king'ora, kikilia kunyamaza,
Hasira macho haina, nafusi huangamiza!

Watu hulewa chakara, kila wakiindeleza,
Wakageuka wakora, wenyewe kujichuuza,
Sio pwani wala bara, huyu ni wazimu pweza,
Hasira macho haina, nafusi huangamiza!

Waume wanadorora, kila ikiwadekeza,
Na wake wanazurura, walipoisindikiza,
Leo wote ni majura, wamebaki kupuuzwa,
Hasira macho haina, nafusi huangamiza!

Nyumbani ikisowera, masinzi hujayasanza,
Na wengine wakagura, utulivu kutukuza,
Vyote haviwi imara, hasira huteketeza,
Hasira macho haina, nafusi huangamiza!

Kazini kuiburura, shari unatengeneza,
Kama maiti hufura, kuzika ukikawiza,
Na harufu huvingira, kunusa hautoiweza,
Hasira macho haina, nafusi huangamiza!

Huyu mama wa hasara, inafaa kumuiza,
Anapoishi kugura, au la atakuchukiza,
Ni kubwa yake madhara, haivishi, huunguza,
Hasira macho haina, nafusi huangamiza!

Ninaiomba nusura, hasira niweze beza,
Anitunuku Ghafura, nimudu kujituliza,
Niwe mtu mwenye dira, nayakwangu  kutengeza,
Hasira macho haina, nafusi huangamiza!


Januari 28, 2012
Kibaha,
Mkoa wa Pwani

No comments: