Thursday, January 12, 2012

Masikio yalokufa

Masikio yalokufa, macho huyasaidia.
Ukaipata sharafa, njiazo kuzitambua,
Ukaepuka maafa, yawezayo kutokea,
Masikio yalokufa, macho huyasaidia.

Hata kama linakufa, hutoacha kusikia,
Utainusa kashfa, kwa macho kuyatumia,
Na hutokosa wadhifa, kwa mengi kuyaelewa,
Masikio yalokufa, macho huyasaidia.

Hakuna cha kuchachafya, akili ukipaua,
Huyarefusha masafa, akili zikasikia,
Macho yakawa ni sifa, usiyojihitajia,
Masikio yalokufa, macho huyasaidia.

Hautaikosa khaifa, hali mtu kuijua,
Na nafasi kwenye dhifa, lazima utajaachiwa,
Huzidisha maarifa, mengi sana ukajua,
Masikio yalokufa, macho huyasaidia.

No comments: