Thursday, January 12, 2012

Shingo isiyogeuka, haimwoni mng'ong'aji!

Kichwa kisichogeuka, hakimwoni mng'ong'aji,
Hivi mtu huepuka, umbeya na usengenyaji,
Njia yako ukaishika, ya nyuma usitaraji,
Shingo isiyogeuka, haimwoni mng'ong'aji!

Na hautoghafilika, kwa unywaji na ulaji,
Hujaliwa kuridhika, ijapo ni mwanamji,
Yasikutishe masika, mafuriko wala maji,
Shingo isiyogeuka, haimwoni mng'ong'aji!

Shingo kutoshughulika, majaribu hutaraji,
Muda huwa muafaka, aghalabu hauufuji,
Na kila unachoshika, faida hautahoji,
Shingo isiyogeuka, haimwoni mng'ong'aji!

Vigumu kushawishika, ukawa ni mfujaji,
Ya kwako huwa hakika, si kama ya mpitaji,
Na nyumba itajengeka,na paa ukahitaji,
Shingo isiyogeuka, haimwoni mng'ong'aji!

Na walioerevuka, si lazima kuwa gwiji,
Vitendo hutambulika, vyenye na visivyo mji,
Na tenzi zikitanzuka, huwa bora watendaji,
Shingo isiyogeuka, haimwoni mng'ong'aji!

No comments: