Tuesday, January 17, 2012

Punje moja

Punje moja ukipewa, unaweza kujaliwa,
Hiyo moja kuja kuwa, eflu za magunia,
Na aliyepewa gunia, kitu kutokuambulia,
Punje moja hujazaa, ikazidi elfu moja.

Viumbe hujaribiwa, kwa hayo wanayopewa,
Vipaji huzawadiwa, tofauti vilokua,
Na kila mshikilia, njia hawezi potea,
Punje moja hujazaa, ikazidi elfu moja.

Kila anayejijua, na mpaji kumwazia,
Shukrani akatoa, na Razaki kumwimbia,
Hana kitachopungua, ila tu kuongezewa,
Punje moja hujazaa, ikazidi elfu moja.

Natunza nilichopewa, uzazi sijaujua,
Mughini namlilia, kustawi vikakua,
Na mimi kuhesabiwa, kati ya waliobarikiwa,
Punje moja hujazaa, ikazidi elfu moja.

No comments: