Friday, January 13, 2012

Nchi ya mangimeza

Nchi ya mangimeza, kila mtu mjuaji,
Viyoyozi wanawaza, na sio utafutaji,
Akili zao za meza, kungoja uandaaji,
Wajanja wakiongoza, na mameneja wajuaji:
Mjanja ni kuchuuzwa,
Na meneja huwauza,
Nuru hugeuka giza,
Amani na nunda humezwa!

Uchumi kujiongoza, haiwi wala haiji,
Watu ngoma wanacheza, na si wahangaikaji,
Twabaki kubangaiza, neema wala haiji,
Wajanja wakiongoza, na mameneja wajuaji:
Mjanja ni kuchuuzwa,
Na meneja huwauza,
Nuru hugeuka giza,
Amani na nunda humezwa!

Watu wataka kufunza, mameneja kuwahoji,
Ovataimu kujuza, huutafuna mtaji,
Shirika huwezi kuza, hata watwae magwiji,
Wajanja wakiongoza, na mameneja wajuaji:
Mjanja ni kuchuuzwa,
Na meneja huwauza,
Nuru hugeuka giza,
Amani na nunda humezwa!

Nchi budi kupooza, wanapoikosa chaji,
Wote tukijilemaza, nani wa kutufariji?
Ushauri wenu viza, nani anauhitaji?
Wajanja wakiongoza, na mameneja wajuaji:
Mjanja ni kuchuuzwa,
Na meneja huwauza,
Nuru hugeuka giza,
Amani na nunda humezwa!

Umeme kifimbo cheza, chama ndio wake mtaji,
TANESCO waumizwa, hali mwingine muuaji,
Laana budi kupaaza, waongo na majuaji,
Wajanja wakiongoza, na mameneja wajuaji:
Mjanja ni kuchuuzwa,
Na meneja huwauza,
Nuru hugeuka giza,
Amani na nunda humezwa!

Shirika wanalicheza, kwa uwizi na ulaji,
Si lazima kujafunzwa, wala kupata ujaji,
Nani utamueleza, asiyekwenda na maji,
Wajanja wakiongoza, na mameneja wajuaji:
Mjanja ni kuchuuzwa,
Na meneja huwauza,
Nuru hugeuka giza,
Amani na nunda humezwa!

No comments: