Sunday, January 29, 2012

Kiongozi roho mbaya

RAIA huwachukia, ukweli wanaomwambia,
Kiongozi roho mbaya, haishi kuchanganyikiwa,
Na kila akiamua, mkenge hachi kwingia,
Kiongozi roho mbaya, raia huwachukia !

Watu atawabagua, wema na wake wabaya,
Kama vile anajua, moyoni yaliyokuwa,
Umungu atajitia, kumbe shetani kamvaa,
Kiongozi roho mbaya, raia huwabagua!

Uongo huusikia, kisha akazingatia,
Kila akikosolewa, vibaya hujisikia,
Badala kuongolewa, hatoacha kupotea,
Kiongozi roho mbaya, ukweli huuchukia !

Nafsi humtangulia, roho ikafuatia,
Kujua akajitia, hata asiyoyajua,
Wenye hoja husinzia, nafasi wakamwachia,
Kiongozi roho mbaya, nafsi hutangulza!

Ujibari hujitia, dhihaka kukomalia,
Mafuu humdhania, akili waliokuwa,
Ila watamuambaa, ahadiye kutimia,
Kiongozi roho mbaya, yake huyafikiria!

Kisasi hukusudia, ukubwa kuutetea,
Hujeruhi na kuua, akachezea dunia,
Na Mola humuachia, madhambi kumwongezea,
Kiongozi roho mbaya, kisasi yake tabia!

Januari 29, 2012
Dar es Salaam

No comments: