Thursday, January 12, 2012

Maganda wanaokula

MACHO huyafungua, na kisu wakakinoa,
Nguvu wakaitumia, maganda kuyaondoa,
Kazi wakimalizia, tunda wanaliachia,
Maganda wanaokula, hufaidi kitu gani ?

Kazi wakimalizia, tunda wanaliachia,
Mezani boi kutia, wazngu wakajilia,
Yesiyesi ikishakua, hakuna chakubakia,
Maganda wanaokula, hufaidi kitu gani ?

Maganda yakibakia, mmenyaji huachiwa,
Kokwa ndani lililokuwa, hilo nalo huachiwa,
Ila nyama wachukua, na hadhi waliokuwa,
Maganda wanaokula, hufaidi kitu gani ?

Utani wajionea, lakini ni kweli huwa,
Ndivo inavyokua, wenyewe tumeamua,
Utumwa tunaanzia, hapa tulipotulia,
Maganda wanaokula, hufaidi kitu gani ?

Babu na bibi wajua, ndio waloanzishia,
Baba na mama pia, nao wamefuatia,
Na watoto tumekua, yale yale yatokea,
Maganda wanaokula, hufaidi kitu gani ?

Uboi twaendelea, mzungu kumtumikia,
Hata nje anapokuwa, vitu tunampelekea,
Na magoti humpigia, na njaa kumlilia,
Maganda wanaokula, hufaidi kitu gani ?

No comments: