Saturday, January 14, 2012

Yao hayawezi dumu

Wa Adi walijaliwa, makubwa kujifanzia,
Na Thamudi nao pia, nyuma hawakubakia,
Hadi walipopotea, wenyewe wakajisifia,
Mungu asiowapenda, yao hayawezi dumu!

Hadi walipopotea, wenyewe wakajisifia,
Na muumba kumtania, madhambi kujipalia,
Kufuru walipozaa, juu walinyanyuliwa,
Mungu asiowapenda, yao hayawezi dumu!

Na chini walipotua, hakuna aliyebakia,
Sauli naye alipewa, akawa ajifikiria,
Wengine kuwatendea, kisichostahilia,
Mungu asiowapenda, yao hayawezi dumu!

Akaonywa hakusikia, Bwana akamsanzua,
Daudi kumchagua, Nabii na dola kutwaa,
Na leo tunajionea, haya waliopugukiwa,
Mungu asiowapenda, yao hayawezi dumu!

Mbwani twajifanyia, Mola anayochukia,
Na ujanja twajitia, kama yeye hatajua,
Huu ujinga tanzia, kujinyonga twaamua,
Mungu asiowapenda, yao hayawezi dumu!

Nadhikiri kuwaambia, badilisheni tabia,
Yaja yakuenguliwa, na mengine mabalaa,
Huruma kuwakimbia, na hasara kuingia,
Mungu asiowapenda, yao hayawezi dumu!

No comments: