Tuesday, January 17, 2012

Januari Ikifika

Elimu sasa sokoni, bajeti yahitajika,
Mwaka huisha taabani, mwanzo wafilisika,
Ila wenye tumaini, pahala wanaposhika,
Januari ikifika, huwa mshikemshike!

Chekechea wamo ndani, fedha inahitajika,
Na msingi kitalini, mikono imenyanyuka,
Sekondari yumkini, nao watingishika,
Januari ikifika, huwa mshikemshike!

Wakiwemo wa Chuoni, na mkopo warauka,
Huwa tena mashakani, mkopo usiposhika,
Huingia akibani, au rehani kuweka,
Januari ikifika, huwa mshikemshike!

Mameneja mashuleni, wenzenu twataabika,
Hebu mpango fanyeni, tarehe zikaachika,
Mbalimbali kubaini, fedha ikagawanyika,
Januari ikifika, huwa mshikemshike!

Katikati naamini, bora kuliko mwanzoni,
Aidha nako mwishoni, sio pa kupaamini,
Nafuu hapo tupeni, tusiwe ovyo nyumbani,
Januari ikifika, huwa mshikemshike!

No comments: