Thursday, January 12, 2012

Chogo kwao ni mbongo, na usogo ni ushamba!

Mshamba niliambiwa, mjini nilipoingia,
Kisa eti sikujua, vifaa kuvitumia,
Kila nikilifikiria, naona huu udhia,
Chogo kwao ni mbongo, na usogo ni ushamba!

Tazama inavyopaa, mpya teknolojia,
Hata na wanaojua, vipo wasivyovijua,
Washamba wakiambiwa, hivi watavumilia?
Chogo kwao ni mbongo, na usogo ni ushamba!

Chogo hudharauliwa, na alwatani wa mtaa,
Ila huja kujaliwa, mali wakajichumia,
Na alwatani wakawa, mwishowe ni vibafrua,
Chogo kwao ni mbongo, na usogo ni ushamba!

Mshamba hunyanyukia, mjuaji kufulia,
Muunguja hufubaa, Mpemba kuja kung'aa.
Ndivyo ilivyo dunia, Alamu mwenye kujua,
Chogo kwao ni mbongo, na usogo ni ushamba!

No comments: