Sunday, January 29, 2012

Utukufu si mazazi

Utukufu sio kazi, wala haijawa ngazi,
Haunao mnunuzi, huchuuzwa mchuuzi,
Viumbe wana ajizi, hilo siyo yao hadhi,
Utukufu si mazazi, utukufu ni majazi!

Ukijisifu mkwezi, na sisi kuwa washenzi,
Liogope jinamizi, na nyuzi zake mkizi,
Mwana mkaa masinzi, majivu wake mpenzi,
Utukufu si mazazi, utukufu ni majazi!

Radhiannu ihifadhi, maisha utangulizi,
Cheo kidata cha ngazi, kung'oka wala si kazi,
Neema sio ujuzi, bali kudrati Muizzi,
Utukufu si mazazi, utukufu ni majazi!

Ninashiba kwazo tenzi, zisizo nayo maudhi,
Naona kama faradhi, kadri ninavyoenzi,
Unapendeza ujuzi, mkuu ukimuenzi,
Utukufu si mazazi, utukufu ni majazi!

Nafsi yangu teuzi, yakidhi masimulizi,
Na jaribu kudarizi, waja wakawa wajuzi,
Wajue pa kukabidhi, na wao wapate majazi,
Utukufu si mazazi, utukufu ni majazi!

Mtukufu mwenye enzi, anipe yake majenzi,
Niuambae ushenzi, udhalimu nao wizi,
Yanisubiri makazi, yenye milele hifadhi,
Utukufu si mazazi, utukufu ni majazi!

Na wala si uongozi, usihomhofu Mwenyezi,
Unaofanya ajizi, dhuluma pia na wizi,
Haki usiomaizi, ila yenye machukizi,
Utukufu si mazazi, utukufu ni majazi!

Haki usiomaizi, ila yenye machukizi,
Na kumuudhi Mwenyezi, kwa wanhyonge uchafuzi,
Nafuu hauongezi, ila madhambi na wizi,
Utukufu si mazazi, utukufu ni majazi!

Nafsi naikabidhi, aitwae mwenye enzi,
Kuiongoza Azizi, katika yake malezi,
Samawati na Ardhi, ipate maangalizi,
Utukufu si mazazi, utukufu ni majazi!


Januari 29, 2012
Dar es Salaam

No comments: