Saturday, January 28, 2012

Maisha kweli mafupi

Maisha mafupi kweli, nimekwishayachungua,
Ni hakika ujahili, vibaya kuyatumia,
Kasiye ya tasihili, kwa dakika hupotea,
Maisha kweli mafupi, ushikalo shikilia,
La, sivyo hujajutia!

Wakati sio kamili, na mwisho hutoujua,
Huwaka kama kandili, na kuzima kama jua,
Kila aliye akili, wahaka utamjaa,
Maisha kweli mafupi, ushikalo shikilia,
La, sivyo hujajutia!

Waishio kibahili, nguvu yao hupotea,
Vikaliwa kihalali, na haramu walokua,
Na mzika Kiswahili, Kingereza humuua,
Maisha kweli mafupi, ushikalo shikilia,
La, sivyo hujajutia!

Penda kilicho kamili, tena ni mia kwa mia,
Ukianza kunakili, fotokopi huungua,
Haitabaki asili, moyoni lililotimia,
Maisha kweli mafupi, ushikalo shikilia,
La, sivyo hujajutia!

Akheri naikabili, kesho yangu sijajua,
Haijanijia dalili, na mwishosijaujua,
Ila ni mustakabali, yafaa kujiandaa,
Maisha kweli mafupi, ushikalo shikilia,
La, sivyo hujajutia!

Ni wangapi marijali, wamekwishatangulai,
Wakiamini amali, baadaye watatoa,
Hakuyataka Adili, mapema kawanyakua,
Maisha kweli mafupi, ushikalo shikilia,
La, sivyo hujajutia!

Ni wangapi wanawali, ujana wameachia,
Walizima ja kandili, utambi kupupuliwa,
Imebakia jamili, hatuishi simulia,
Maisha kweli mafupi, ushikalo shikilia,
La, sivyo hujajutia!

Januari 28, 2012
Kibaha,
Mkoa wa Pwani

1 comment:

Godfrey Mutuli said...

Maisha mafupi kweli,ushikalo shikilia.