Thursday, January 12, 2012

Miwani mingine ramli

Miwani mingine ramli, huonwa na ruia,
Na wepesi wa kauli, hili huja simulia,
Kwa utelezi wa samli, hoja ikakubaliwa,
Miwani mingine ramli, huonwa tusiyojua!

Miwani mingine ramli, mganga kakupigia,
Wewe ukajua kweli, kisicho kung'ang'ania,
Wafanyao bilkuli, kujua ukakataa,
Miwani mingine ramli, huonwa tusiyoona!

Nafsi za kijahili, mazuri hutarajia,
Hata zikipanda wali, kuvuna hutegemea,
Na wasio idhilali, hili hawatoliridhia,
Miwani mingine ramli, huonwa tusiyojua!

Utu wataka kubuli, na imani kujaliwa,
Hukataa mushkeli, sembuse wizi ukawa,
Huyauliza maswali, kabla feli kuivaa,
Miwani mingine ramli, huonwa tusiyoona!

Elektroniki ghali, kwa ujumbe ukitoa,
Hukugharimu ukweli, uongo ukiumbuliwa,
Zitupwe ardhilhali, huko zinakotokea,
Miwani mingine ramli, huonwa tusiyoona!

Na uji sio ugali, nani kukukubalia?
Uji maji yake hali, na ugali unaliwa,
Bure ukiwa mkali, kitu budi chapungua,
Miwani mingine ramli, huonwa tusiyoona!

Kiumbe nisiye hali, nafaa kuhurumiwa,
Nayataka ya Jalali, nusura inayoongoa,
Si ya ndumilakuwili, shiriki anayetia,
Miwani mingine ramli, huonwa tusiyoona!

Kwa hao mimi bahili, japo ninalia njaa,
Naitafuta kandili, wengi sana kuyajua,
Japo ni dhoofu hali, lazima mtayajua,
Miwani mingine ramli, huonwa tusiyoona!

No comments: