Monday, January 9, 2012

WAPANGAJI WAKIMBIZI

UBEPARI ni unyama, jana Kenya ilikuwa,
Na leo watu wazima, hukohuko twaingia,
Tumeikosa huruma, hata kwa walio wakiwa,
Hii ndio nchi yetu, wapangaji wakimbizi.

Mshairi natetema, mateso kufikiria,
Wazee watu wazima, baridi yawaingia,
Watoto waso lawama, hatiani waingia,
Hii ndio nchi yetu, wanye nyumba ni wenzetu!

Facebook nawasema, huruma mnatakiwa,
Yafanyeni ya ujima, wapangaji kuwafaa,
Waondokane nakama, kwa muda wakatulia,
Hii ndio nchi yetu, wenye nyumba watu wetu.

Atawajaza karima, mje nanyi kuhurumiwa,
Penye adha za kiyama, kivulini mkatiwa,
Na nyingi sana rehema, duniani mkapewa,
Hii ndio nchi yetu, wapangaji si wenzetu!

Kwa ya wakubwa kalima, ukweli tumegundua,
Kumbe nchi inachuma, madhambi yaliyojaa,
Wapi tupate salama,akitukasirikia?
Hii ndio nchi yetu, wapangaji wakimbizi.

Tufanye ima fa ima, wapangaji waugua,
Wanaikosa heshima, na utu kuwapungua,
Tusiishie kutazama, twende kuwasaidia,
Hii ndio nchi yetu, wanye nyumba ni wenzetu!

Ni ipi kubwa gharama,sisi tunaihofia?
Kuliko wa kwetu umma, maisha kuyaokoa,
Kigugumizi nakwama, nashindwa wasimulia,
Hii ndio nchi yetu, wenye nyumba watu wetu.

Nyumba kitu cha lazima, binadamu kupatiwa,
Ni wasio na hekima, hili watanibishia,
Wanatisha maamuma, ukweli wasiojua,
Hii ndio nchi yetu, wapangaji si wenzetu!

No comments: