Raundi ya kwanza yesha, ya pili tunaingia,
Inafaa kujipasha, kazi iliyobakia,
Ni uchumi kuegesha, pale inapotufaa,
Sekan'rauni, Mapinduzi Zanzibar.
Bandari za kuegesha, meli zinahitajiwa,
Kupakia na kushusha, kituo kikuu kuwa,
Kiswe kiwe komesha, kama mwanzo wa dunia,
Sekan'rauni, Mapinduzi Zanzibar.
Garimoshi kujitwisha, magari yakapungua,
Kaskazini kushusha, kusini likaingia,
Magharibi kuliwasha, matlai likatua,
Sekan'rauni, Mapinduzi Zanzibar.
Garimoshi lisochosha, umeme litatumia,
Tuzidi linaksisha, hata jua kutumia,
Mazingira kutoshusha, hadhi tuliyopatia,
Sekan'rauni, Mapinduzi Zanzibar.
Uwanja ndege kushusha, Dubai unaozidia,
Mizigo kujaishusha, Afrika kuingia,
Yapande yetu maisha, Waarabu kushangaa,
Sekan'rauni, Mapinduzi Zanzibar.
Ndege budi kukodisha, Kwa Air Zanzibar,
Vijana kuelimisha, urubani kuujua,
Na injini kuzishusha, mentenesi kufanzia,
Sekan'rauni, Mapinduzi Zanzibar.
Hospitali kuboresha, lazima kuazimia,
Comoro kuteremsha, wagonjwa kuja tibiwa,
Huduma kurefusha, Tanganyika kuingia,
Sekan'rauni, Mapinduzi Zanzibar.
Madaktari wa kutosha, ni lazima kuwalea,
Kama Cuba kuonyesha, maajabu kwa dunia,
Mapato kujineemesha, Zanzibar ikapaa,
Sekan'rauni, Mapinduzi Zanzibar.
Shule twaweza boresha, kimataifa zikawa,
Na walimu kuwashusha, Ulaya kuwavutia,
Pia kwa yake maisha, Uarabuni nao pia,
Sekan'rauni, Mapinduzi Zanzibar.
Visiwa viwe tamasha, shule bora ya dunia,
Watu wote kusomesha, mbalimbali tasnia,
Mapato kuyarefusha, na upana kupanua,
Sekan'rauni, Mapinduzi Zanzibar.
Vingi twaweza anzisha, kwa nchi kama kisiwa,
Golfu kuirejesha, kimataifa ikawa,
Formula 1 kushusha, mbio wakazitumua,
Sekan'rauni, Mapinduzi Zanzibar.
Manani atatuvusha, muhimu kukusudia,
Ufakiri utaisha, na utu wetu ukawa,
Dunia tukawakosha, wazidi kututembelea,
Sekan'rauni, Mapinduzi Zanzibar.
Thursday, January 12, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment