Ujana uliponiumbua,
Hali pekee nimebakia,
Wewe ndiye uliyenifaa,
Yakini ukanihurumia,
Na vyema kunihudumia,
Nusu maiti nilishakua,
Maajabu ukanifufua:
Asia !
Matatizo uliyapokea,
Changamoto kwako kuchukua,
Na dhiki ukaivumilia,
Kwa mzigo uliochukua,
Kitanda ukanitandikia,
Na nguo mwilini kunivua,
Kulala chini ukabakia:
Asia !
Wasema nilikusaidia,
Ila wewe ndio ulonifaa,
Kaitka hii yetu dunia,
Mwingine sijashuhudia,
Uzuri uliojaliwa,
Mwengineo sijajionea,
Ni adimu uliyonigawiya:
Asia !
Wema kweli wanahesabiwa,
Kwa idadi yao walivyokua,
Najivuna nawe ulikuwa,
Kati ya wanaohesabiwa,
Ingawa machoni wapotea,
Moyoni nimekwishakujengea
Ghorofa ya dhahabu yang'aa:
Asia !
Na machoni nisipokutia,
Hadi nitakapokujajifia,
Urulaini nakutumainia,
Wangu mmojawao utakua,
Macho yako ya kusinzia,
Haifai kuja kupotea,
Milele mimi nawe kukaa:
Asia !
S.M.
Kolila, Old Moshi, 1977
Tuesday, January 10, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment