Thursday, January 12, 2012

Salamu za malkia

MADOLA mmeamka, asubuhi yaingia,
Jogoo ameshawika, kuamka mnatakiwa,
Uchumi kuja kushika, imara ukarejea,
Salamu namtumia, Malikia wa madola.

Udugu tumeushika, nyuma hatutarejea,
Na mengi uliyotaka, hakika yametimia,
Ila hatua twataka, njaa ipate potea,
Salamu namtumia, Malikia wa madola.

Tumejenga ushirika, hali twaziangalia,
Na palipo na mashaka, hatwachi shughulikia,
Ila tuache kunyuka, wasio nayo hatia,
Salamu namtumia, Malikia wa madola.

Ajira tuanzitaka, sasa kwetu ni udhia,
Twasoma bila kuchoka, ila kazi zinapotea,
Mikakati kuiweka, hili kuja litatua,
Salamu namtumia, Malikia wa madola.

Mambo mengi yafanyika, London kuinyanyua,
Isikose Afrika, nayo pa kujinasua,
Huu ndio wetu mwaka, vikwazo kuviondoa,
Salamu namtumia, Malikia wa madola.

Elimu yashaurika, iwe inayotumiwa,
Matatizo kuyasaka, na kisha kuyaondoa,
Kwani hili likifanyika, tutapiga kubwa hatua,
Salamu namtumia, Malikia wa madola.

Mathalani tutaamka, reli kujenga upya,
Na vichwa tukavisuka, hapa nyumbani tukiwa,
Ajira zikatanzuka, na nchi kuendelea,
Salamu namtumia, Malikia wa madola.

Malkia kutushika, kwayo tunatazamia,
Kauli ikiitaka, hapamengi yatakua,
Na hapa Afrika, ijivune Tanzania,
Salamu namtumia, Malikia wa madola.

No comments: