Saturday, January 21, 2012

Kupika sasa gharama

Nahamia hotelini, kupika sasa gharama,
Bado twateta chumbani, kuhusu hii azma,
Twahofia inflesheni, njaa kuja tusakama,
Kupika sasa gharama, nahamia hotelini!

Kupika sasa gharama, nahamia hotelini!

Ingawa nautamani, wali wa nazi kuwama,
Robo yazidi thamani, mshahara siku nzima,
Siwezi nimebaini, sintofika mwezi mzima,
Kupika sasa gharama, nahamia hotelini!

Majirani kwaherini, hotelini nahamia,
Mtu kuwa mashakani, naona hii dhuluma,
Hali hii si utani, kama hauna neema,
Kupika sasa gharama, nahamia hotelini!

Hotelini kuhamia, sahani nusu twagawa,
Mchuzi huongezewa, japo maji wametia,
Na siku itaingia, na kesho kuamkia,
Kupika sasa gharama, nahamia hotelini!

Mkaa sintanunua, elfu tatu kwa fungu,
Nyanya nitaachia, wahindi nao wazungu,
Na hayo mafuta taa, redioni kuyasikia,
Kupika sasa gharama, nahamia hotelini!

Mafuta ya kupikia, nitayakwepa kabisa,
Ila kwa kujipakia, badala yenye anasa,
Na chumvi sintonunua, ila kwa kujichulia,

Harufu mbaya nyumbani, sasa itajapungua,
Na nzi watabaini, wenyewe wakaishia,
Usafi tutauwini, nuru nyumba ikajaa,
Kupika sasa gharama, nahamia hotelini!

Mwana kuja kuungua, tena siwezi hofia,
Nitazikwepa balaa, nyingi zinazotokea,
King'amuzi kukivaa, hata mchana ikiwa,
Kupika sasa gharama, nahamia hotelini!

Kisu niache tumia, na makali kuhofia,
Ila matunda yakiwa, shambani yametokea,
Kumenya nitamuambia, mama watoto kuzua,
Kupika sasa gharama, nahamia hotelini!

Na kisha kujisomea, muda sintopungukiwa,
Shahada kuiwania, ufukara kukataa,
Ni heri iliyokuwa, wengi hatujaijua,
Kupika sasa gharama, nahamia hotelini!

Bei zikijapungua, nitakuwa niahapoa,
Huko tena kurudia, ni vigumu itakuwa,
Mteja nitabakia, kwa raha kuizoea,
Kupika sasa gharama, nahamia hotelini!

No comments: