Mchawi wake ni nani, fukuza hizi vyuoni,
Tunapata kitu gani, wanyonge tukiwahini,
Huu ni ukubwa gani, dhiki kutozithamini?
Fukuza, fukuza vyuo, mchawi wake ni nani?
Naona uhayawani, kuua aliye duni,
Unyama sasa imani, tayari tumesaini,
Na laana ni za nani, kumwangukia kichwani?
Fukuza, fukuza vyuo, mchawi wake ni nani?
Wafukuzwao vyuoni, waishiapo kuwalaani,
Yawafika mambo gani, nyie na wana ndani,
Nahisi ni nuksani, na fedheha duniani,
Fukuza, fukuza vyuo, mchawi wake ni nani?
Waneshanuna mbinguni, kilio kukibaini,
Maisha yenu amini, hayanao udhamini,
Mtakuwa mashakani, mjini na vijijini,
Fukuza, fukuza vyuo, mchawi wake ni nani?
Tunaweza yumkini, kuacha ufukuzani,
Haki tukiithamini, na ya utu kuamini,
Tusiwe malimbukeni, tukazidi jiamini,
Fukuza, fukuza vyuo, mchawi wake ni nani?
Kizazi chataka wini, usawa kuubaini,
Wasifanzwe majinuni, nchini ni wahaini,
Na wanaotathmini, wafanya uhayawani,
Fukuza, fukuza vyuo, mchawi wake ni nani?
Atatufunza Manani, kama si leo mwakani,
Hujinadi majivuni, alokua afkani,
Akaishia zawiani, wamuone kama nyani,
Fukuza, fukuza vyuo, mchawi wake ni nani?
Thursday, January 12, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment