Wednesday, February 1, 2012

Swali la wakati wetu

Nchi inadidimia, wakubwa waifagia,
Juu wataka bakia, hata ngazi pasokuwa,
Na sakafu yatitia, wao wanashindilia,
Swali la wakati wetu, posho au bila posho ?

Haya wasioijua, wataka kuazimia,
Bila ya kuzingatia, kilio tunacholia,
Yatima tumebakia, hakuna wa kutufaa,
Swali la wakati wetu, posho au bila posho ?

Wakubwa kulia njaa, uchuro huu balaa,
Hali wadogo wajua, matumbo wanapepea,
Hamjui mwenye njaa, wa shibe anaaminia,
Swali la wakati wetu, posho au bila posho ?

Mizani wakitumia, daima imepungua,
Nchi walipoanzia, mbele watatu adawa,
Hamsini kutimia, ni maadui kadhaa!
Swali la wakati wetu, posho au bila posho ?

Hali halisi kujua, nyie sana mwatakiwa,
Sio mambo kuamua, kama mu kwenye kisiwa,
Ya wengine kutojua, ila mnayoyalilia,
Swali la wakati wetu, posho au bila posho ?

Hivyo mkijifanyia, imani itapotea,
Wananchi kuwakataa, bungeni kutorudia,
Na milele kuhisiwa, yote mabaya yakawa,
Swali la wakati wetu, posho au bila posho ?

Kama hamjautoa, umaskini ulokuwa,
Vipi mnaongezewa, msichokwishatuongezea?
Ila njaa na kut'ua, wenyewe mkabakia?
Swali la wakati wetu, posho au bila posho ?

Kazi mkjifanyia, bila kitu kwongezea,
Haifai kujapewa, juu chochote kikiwa,
Wajibu haujatimia, hapo mtatuibia,
Swali la wakati wetu, posho au bila posho ?

Wabunge mnatakiwa, jambo hili kulijua,
Watumishi nao pia, nchi wanaotumikia,
Posho mliyokipewa, sasa ya kuondolewa,
Swali la wakati wetu, posho au bila posho ?

Ila mtakapoyazua, wananchi yakawafa,
Kipato kuwaongezea, na shida kuwaondolea,
Bonasi mtapokea, tena kubwa zilokuwa,
Swali la wakati wetu, posho au bila posho ?

Februari 1, 2012
Dar es Salaam

No comments: