Sunday, February 26, 2012

Usitende bila fikra

Mnyama ungelikuwa, sawa tungelidhania,
Mambo kutofikiria, na kisha ukayaingia,
Utu yende kukuvua, na uchi ukabakia,
Usitende bila fikra, waza kabla kutenda!

Fikra ni majaliw,a mja amezawadiwa,
Yafaa kufikiria, kabla haujaamua,
Na utenzi hutanguliwa, kwa mawazo yalokuwa,
Usitende bila fikra, waza kabla kutenda!

Amri kuzipokea, ukatenda usojua,
Wewe umelaaniwa, na mbingu na ardhi pia,
Na moto wa kungojea, hunalo la kujitetea,
Usitende bila fikra, waza kabla kutenda!

La haki lililokuwa, kulitenda inafaa,
Na haki lisilokuwa, ni wajibu kukataa,
Muogopeni Jalia, si watu kuwahofia,
Usitende bila fikra, waza kabla kutenda!

No comments: