Monday, February 20, 2012

Pato linakwenda wapi

Kila siku tunaliwa, na wao zinaingia,
Wanakuwa bilionea, na sisi hatuna shea,
Na bodi sijasikia, kamari kusimamia,
Pato linakwenda wapi, kamari za kwenye simu?

Mapesa naulizia, huko utakapokuwa,
Hesabu unazijua, kiasi kinachoingia,
Ni wapi zinaingia, na nani zamsaidia,
Pato linakwenda wapi, kamari za kwenye simu?

Au wenyewe watanua, kwa magari kununua,
Minara kujijengea, na fedha kujiwekea,
Wao tajiri wakawa, sisi masikini kuwa ?
Pato linakwenda wapi, kamari za kwenye simu?

Kiasi wanachukua, si kidogo nakwambia,
Na zuzu tulivyokuwa, kila mmoja adhania,
Yere ndiye atakuwa, siku hiyo milionea,
Pato linakwenda wapi, kamari za kwenye simu?

Hadhari hawajatoa, wacheza kuzingatia,
Yaweza kuja ikawa, bahati nasibu ubaya,
Fakri wakazimia, na wengine kujiua,
Pato linakwenda wapi, kamari za kwenye simu?

Fakri wakazimia, na wengine kujiua,
Umaskini kizidia, pasiwe wa kuwakwamua,
Zikabaki familia, zazidi kuteketea,
Pato linakwenda wapi, kamari za kwenye simu?

Wenye dini wanajua, haramu yatambuliwa,
Kucheza haitofaa, umaskini inatia,
Serikali yaachia, kwa yale inayojua,
Pato linakwenda wapi, kamari za kwenye simu?

Ni wahuni wamejaa, mambo wajifanyia,
Mitaani waingia, hakuna wa kuwafatia,
Au pengine watuvaa, ubia wameuchukua?
Pato linakwenda wapi, kamari za kwenye simu?

Mashaka inantia, hali inavyoendelea,
NI kiwanja kimekua, kila mcheza kwingia,
Na fujo kujifanyia, asiwe wa kuadhibiwa,
Pato linakwenda wapi, kamari za kwenye simu?

Wachache wajilimbikia, mamilionea kuwa,
Sisi tunadidimia, ustawi watokomea,
Hata tulichojiokotea, nacho wanakichukua,
Pato linakwenda wapi, kamari za kwenye simu?

No comments: