Wednesday, February 22, 2012

Sisi tunamalizia

FIKRA hatukupewa, kioto tunatumiwa,
Sheria zilizovia, za ukoloni kuzaa,
Leo anaziambaa, atii demokrasia,
Mwakataa kuuawa, sasa tunamalizia!


Bado inalingojea, katiba kuliondoa,
Sasa linalotakiwa, nchini kutoendelea,
Huria watu wakawa, kuandamana na njia,
Mwakataa kuuawa, sasa tunamalizia!

Dukuduku kuzitoa, na goigoi kufichua,
Na ndiyo pekee njia, raia ameachiwa,
Vinginevyo huzuiwa, uhuru nao usawa,
Mwakataa kuuawa, sasa tunamalizia!

Ataamini kichaa, garijeshi kuvamiwa,
Uongo mnaozua, saizi mnapimia?
Roho zitawalilia, hata kama mwatumiwa,
Mwakataa kuuawa, sasa tunamalizia!

Nchi yataka ulua, raia kuangalia,
Yao watayoamua, kulindwa nazo sheria,
Si kila mkuu wa mkoa, maguvu kuyatumia,
Mwakataa kuuawa, sasa tunamalizia!

Hatua mwanzo zafaa, na sio kuyangojea,
Mabaya yakatokea, kwa nyie mnapochelewa,
Maamuzi kuchukua, na usalama ukawa,
Mwakataa kuuawa, sasa tunamalizia!

Ujumbe mlioutoa, ndivyo hivi natambua,
Haki anayelilia, sasa atashindiliwa,
Siasa tunaitia, hata isipotokea,
Mwakataa kuuawa, sasa tunamalizia!

Hawa tunaoteua, yabidi kuangalia,
Uchama ukizidia, taifa wataliua,
Fikra mgando kuwa, basi hili kubwa baa,
Mwakataa kuuawa, sasa tunamalizia!

Songea nawalilia, kwa ndugu waliopotea,
Mungu atawajali, uchungu kuuondoa,
Na wakuu kupatiwa, hali wanaowajua,
Mwakataa kuuawa, sasa tunamalizia!

Ya rabi watusikia, watazame wa Songea,
Uhai waondolewa, kushoto pia kulia,
Ni wewe twatarajia, jahazi kuliokoa,
Mwakataa kuuawa, sasa tunamalizia!

No comments: