Monday, February 27, 2012

RAIS AWE MWANAMKE!

Mbili ziro moja tano


KWA MIAKA hamsini, wanaume wanapewa,
Waja hadi utosini, hakuna linalokuwa,
Wameshindwa yaniyani, mimi mmoja nikiwa:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!


Nyerere wa kwanza kawa, twamshukuru radhia,
Mazuri katufanyia, na mabaya nayo pia,
Islamu twatambua, ila twajinyamazia:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Mwinyi alipoingia, makubwa tulidhania,
Hivyo katu haikuwa, palepale twabakia,
Ila njaa kupungua, twampa asante hewaa,
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Mkapa kumpokea, kisasi tunakijua,
Lipi lililotufaa, ila yao yalokuwa,
Ila barabara hewaa, sasa tunaitumia:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Wengine watuchagua, maua tumeshakua,
Ila nchi yasogea, nyuma mbele hatujajua
Sasa hali imekuwa, mbaya kwa tusiokuwa:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Vjijini wanalia, ugumu umezidia,
Na maji yamepotea, japo waliahidiwa,
Kuni zinawakimbia, zaenda zinakokua:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Na mjini nako pia, familia zateketea,
Baba wanazikimbia, ugumu ulivyokuwa,
Asema twaendelea, siriye hatujaijua:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Matatizo yalokuwa, wanawake wayajua,
Ndio yanyowavaa,asubuhi kuanzia,
Hadi jioni kwingia,hakuna wa kupumua:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Waume watuzidia, wezi wanavyoujua,
Na uongo wakatoa, kweli ukawakubalia,
Mwanamke akiingia, wizi budi kupungua:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Ufisadi nakwambia, mwanamke hukimbia,
Wengine hufikiria, watakavyokujaumia,
Halali hukimbilia, na haramu kukataa:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Trafiki ukitoa, rushwa wanaikataa,
Labda wanapotumiwa, na wanasiasa wakiwa,
Ila ya fedha baa, hili wanalitambua:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Matanuzi huambaa, na wanaume si sawa,
Ubadhirifu hadaa, vya watu utavitumia,
Hili wanalitambua, na kufanya ni nazaa:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Angalia Liberia, sasa inaendelea,
Wivu tu unawajaa, wanaume wasopewa,
Haweshi kuyazomea, mazuri yaliyokuwa:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Argentina tulia, nao nakuelezea,
Uchumi sasa wakua, mzee kujiondoa,
Na hata alipojifia, nchi yajititimua:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Ukenda Australia, mama anashikilia,
Dume limeondolewa, kwa kuuzusha udhia,
Uchumi wao wapaa, dunia inashangaa:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Nafuu natamania, miaka kumi ikawa,
Nyumbani wakabakia, wanaume mabalaa,
Ili kuiangalia, Tanzania itavyopaa:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

Ili kuiangalia, Tanzania itavyopaa,
Mama rais akiwa, na watu kuwanyanyua,
Sijali atatokea, chama gani kilichokuwa:
Mbili ziro moja tano, Rais wa Tanzania:
Budi awe mwanamke!

No comments: