Monday, February 20, 2012

Mwalimu kulaumiwa

WEPESI kuwatumia, watu wengine lawama,
Na sisi kufikiria, madoa tumeyahama,
Ushahidi ulokuwa, sote ni wenye nakama,
Mwalimu kulaumiwa, 'skepugoti' amekua,
Mbona mchawi twamjua,
Vitabu aleta yeye?

Malaika hajakuwa, mwalimu akasimama,
Afanye asiyojua, na kuzishusha neema,
Mwenyewe akachanua, kwa wengine kuwa mwema,
Mwalimu kulaumiwa, 'skepugoti' amekua,
Mbona mchawi twamjua,
Majengo anaboresha?

Ni kinyaa yamekuwa, madarasa tumekwama,
Huwezi kufanania, ya TV kutazama,
Hata wasioendelea, watupita kwa kilima,
Mwalimu kulaumiwa, 'skepugoti' amekua,
Mbona mchawi twamjua,
Madarasa ayapamba ?

Shule hazina vifaa, mabohari kutazama,
Kitu yasiyokuwa, yanangojewa kuazimwa,
Akili tupu hukua, ndani ukiyatazama,
Mwalimu kulaumiwa, 'skepugoti' amekua,
Mbona mchawi twamjua,
Vifaa aleta yeye?

Chini wanajiketia, na kuandika tuhuma,
Mtoto ukimuwazia, kwa shida sana asoma,
Aona aadhibiwa, tena hapewi heshima,
Mwalimu kulaumiwa, 'skepugoti' amekua,
Mbona mchawi twamjua,
Madawati yako wapi?

Supavaisa wapotea, ubora nani kupima,
Hawa wanapotokea. pengine ni mwaka mzima,
Wakati inatakiwa, kufuatia kwa daima,
Mwalimu kulaumiwa, 'skepugoti' amekua,
Mbona mchawi twamjua,
Udhibiti uko wapi ?

Madai yazidi kua, kulipwa bado zahama,
Hata ukijifikiria, hili halina ulama,
Kisa utakitambua, cha miguu kuzizima,
Mwalimu kulaumiwa, 'skepugoti' amekua,
Mbona mchawi twamjua,
Malipo yao ya wapi?

Nyumba ukiwapatia, ni ipi kubwa gharama,
Akili ikitumiwa, rahisi na kitu chema,
Ila wasiojitegemea, hutafuta ya kukwama,
Mwalimu kulaumiwa, 'skepugoti' amekua,
Mbona mchawi twamjua,
Nyumba za kuishi wapi?

Vijana tukiwatumia, mengi twaweza kuchuma,
Mzungu kumtegemea, hatutaisha kuzama,
Akili tukipungua, twakitafuta kilema,
Mwalimu kulaumiwa, 'skepugoti' amekua,
Mbona mchawi twamjua,
Maslahi yako wapi?

Uhuru tulipotwaa, ilikuwepo heshima,
Na mwalimu kujaliwa, akajiona ni mwema,
Leo tuanwachukia, kwa dharau kuwasema,
Mwalimu kulaumiwa, 'skepugoti' amekua,
Mbona mchawi twamjua,
Heshima yao iwapi?

Watoto walijijua, mwalimu kweli ulama,
Wakawa wamwamkia, na kazi wakajituma,
Mwalimu wakamfaa, huku akazana kusoma,
Mwalimu kulaumiwa, 'skepugoti' amekua,
Mbona mchawi twamjua,
Utu wao ukowapi ?

Kazi kumsaidia, kwake jioni wasoma,
Udugu kujijengea, wakawa moja jamaa,
Leo tunashushuliwa, na kujenga uhasama,
Mwalimu kulaumiwa, 'skepugoti' amekua,
Mbona mchawi twamjua,
Wao sio binadamu ?

Mola ninamliliya, mwenye wingi wa huruma,
Walimu kutuangalia, taifa kulitazama,
Kweli tunayongojea, malipo yaliyo mema,
Mwalimu kulaumiwa, 'skepugoti' amekua,
Mbona mchawi twamjua,
Mwala nyie, wakose wao ?

No comments: