Sunday, February 26, 2012

Umeme unapozima

Kwenye nchi ya madoa, rangi tusiyoyajua,
Na amri za kuua, wadhani hawajaua,
Na yatakiwayo kuwa, yasiwe yenye kukua,
Umeme unapozima, na giza likaenea:
Mwangaza hunifunua,
Utunzi nikaingia,
Hadi adhana ikawa!


Ukuu wanaochukua, wasiwe pakuanzia,
Na wanaoyachimbua, wakadhani walimia,
Huwa nchi ya wafukua, kuzikwa kwao haijawa,
Umeme unapozima, na giza likaenea:
Mwangaza hunifunua,
Utunzi nikaingia,
Hadi adhana ikawa!


Ndipo saa wazijua, kizani kutususia,
Mengi yananipitia, pembeni nilipokaa,
Wasiojua wajua, ndiyo nchi imekuwa,
Umeme unapozima, na giza likaenea:
Mwangaza hunifunua,
Utunzi nikaingia,
Hadi adhana ikawa!


Hakuna wa kutumiwa, wote wataka tumia,
Kuvuna washangilia, kupanda wanakataa,
Wachache hupalilia, nao mimea hung'oa,
Umeme unapozima, na giza likaenea:
Mwangaza hunifunua,
Utunzi nikaingia,
Hadi adhana ikawa!


Nchi ya wasiojijua, na kwendako wapotea,
Taifa lisilojifua, kutakata haijawa,
Na uchafu waujua, tena wanautumia,
Umeme unapozima, na giza likaenea:
Mwangaza hunifunua,
Utunzi nikaingia,
Hadi adhana ikawa!


Watu wa kusaidiwa, wasiojisaidia,
Nchi yenye kununua, chake isichokizaa,
Ni nchi ya kulaniwa, mbele haitoendelea,
Umeme unapozima, na giza likaenea:
Mwangaza hunifunua,
Utunzi nikaingia,
Hadi adhana ikawa!


Nchi ya viguu na njia, haiwezi kutulia,
Yao wasiotatua, ya wengine wakavaa,
Ni ya kusikitikiya, na tena kuhurumiwa,
Umeme unapozima, na giza likaenea:
Mwangaza hunifunua,
Utunzi nikaingia,
Hadi adhana ikawa!


Ndio ninafurahia, umeme ukisinzia,
Huamka na kuzua, visa vya kuhadithia,
Kizazi kitachokuwa, haya kuja yaambaa,
Umeme unapozima, na giza likaenea:
Mwangaza hunifunua,
Utunzi nikaingia,
Hadi adhana ikawa!

No comments: