Sunday, February 19, 2012

Kukuwa kwa mbilikimo

Huo ni wao msemo, hutapika kukohoa
Uongo chao kipimo, hakunaasiyejua,
Lakini wenye kisomo, kweli hawajagundua,
Kukuwa kwa mbilikimo, si sawa na Goliath!

Asifiwa mbilikimo, eti sana amekua,
Kumbe pale aliomo, jiwe amesimamia,
Ukishuka mtetemo, ni chini huangukia,
Kukuwa kwa mbilikimo, si sawa na Goliath!

Viatu vya mchuchumo, mbilikimo amevaa,
Waonao kwa ukomo, waona sasa kakua,
Mapambo kumpambia, asiyoyastahilia,
Kukuwa kwa mbilikimo, si sawa na Goliath!

Wanazifanya nderemo, kweli hali waijua,
Hajakua kwa kipimo, sote tunachokijua,
Mazingaombwe yamo, na nani asiyejua?
Kukuwa kwa mbilikimo, si sawa na Goliath!

Hawa wepesi wa domo, masafi kuyakamia,
Na chao kidomodomo, sasa kwa wengi udhia,
Umma wataka msukumo, wala si kusukumiwa,
Kukuwa kwa mbilikimo, si sawa na Goliath!

Makongoti mbilikimo, wamwambia nenda vaa,
Na sasa yuko kwenye mgomo, breki zinakataa,
Gari halina ngurumo, injini imetulia,
Kukuwa kwa mbilikimo, si sawa na Goliath!

Mara washika kilimo, mara wajaliachia,
Ninasikia msukumo, sasa sumu kuchimbua,
Mhemuko ndio somo, twavaa tusichovua ?
Kukuwa kwa mbilikimo, si sawa na Goliath!

Na sasa kuna ngurumo, akili zisizopewa,
Haiendani mifumo, kwa wengine kupakua,
Nchi yataka kisomo, asili kuichimbua,
Kukuwa kwa mbilikimo, si sawa na Goliath!

Februari 20, 2012
Dar es salaam. Tanzania

No comments: