Monday, February 20, 2012

Watu wazima kufanzwa watoto

HUGEUZWA ni watoto, wakaamrishwa kuimba,
Hawafunzwi maliwato,dawa waenda kuchimba,
Mambo yao zimamoto,maji yakisha hutamba,
Watu wazima yatisha, kufanywa kuwa watoto,
ama njaa yasumbua!

Wakubwa kuota ndoto,za kuteta na kugomba,
Wawe wapigana ngoto,na vikumbo kuvikumba,
Huashiria mazito, ya kuja katika kamba,
Watu wazima yatisha, kufanywa kuwa watoto,
ama njaa yasumbua!

Akili zenye utoto, fikra zina ugumba,
Hazijengi yenye woto, mizizi haiwi gamba,
Mjukuu si majuto, majuto kutojichamba,
Watu wazima yatisha, kufanywa kuwa watoto,
ama njaa yasumbua!

Akili si kama puto, kuliacha likawamba,
Liende kusiko pato, kwa mjini au shamba,
Maisha sasa makato, hakuna anayetemba,
Watu wazima yatisha, kufanywa kuwa watoto,
ama njaa yasumbua!

Hatudharau watoto, ila hilo lao gamba,
Huibadili fukuto, tabia zinajiumba,
Mengineyo ni mapito, ngazi zenye kujiremba,
Watu wazima yatisha, kufanywa kuwa watoto,
ama njaa yasumbua!

Hali zdtu ni mseto, tufani zaweza kumbwa,
Zikapoteza mvuto, tusiwe tunaoimbwa,
Majina yawe mkato, historia ikafumba,
Watu wazima yatisha, kufanywa kuwa watoto,
ama njaa yasumbua!

Wazima kuwa watoto, wakafundishwa kuimba,
Yananipa tumbo joto, utumbo waweza vimba,
Utafariki mchakato, kufa tusivyoviumba,
Watu wazima yatisha, kufanywa kuwa watoto,
ama njaa yasumbua!

No comments: