Tuesday, February 28, 2012

Ya nchi yanatushinda

UKISHAJITEGEMEA, ya wengine angalia,
Sio unategemea, uwezo ukajitia,
Msaada ukipungua, na wengine huumia,
Ya nchi yanatushinda, twafata ya ulimwengu?

Ndivyo nchi yatakiwa, mambo yake kupangia,
Sio ikajishushua, kuvaa itakayovua,
Bila ya kuendelea, wasanii mnakua,
Ya nchi yanatushinda, twafata ya ulimwengu?

Moja, mbili, tatu kuwa, hesabu inayotakiwa,
Huwezi ukarukia, kwingine ukavamia,
Huonekana kichaa, au mwehu umekuwa,
Ya nchi yanatushinda, twafata ya ulimwengu?

Kimbelembele tukiwa, wenyewe tutaumia,
Fashioni haijawa, shoo ya kutoendelea,
Kufanywa yanatakiwa, sio ya kuhadithia,
Ya nchi yanatushinda, twafata ya ulimwengu?

Nchi ikishaendelea, wengine inavutia,
Kamba hautochukua, kuvuta ukang'ang'ania,
Wenyewe wataingia,ya kwao wakachagua,
Ya nchi yanatushinda, twafata ya ulimwengu?

Taifa likishakua, heshima huzawadiwa,
Watalii wakapaa, na kuja hapa kutua,
Ndarahma kutwachia, zikawa na manufaa,
Ya nchi yanatushinda, twafata ya ulimwengu?

Zikitumika sheria, si ubabe kutumiwa,
Wote kushughulikiwa, bila ukubwa kutia,
Wote kujiinamia, katiba kuangukia,
Ya nchi yanatushinda, twafata ya ulimwengu?

Njiani tukitembea, pasiwe juu wakaa,
Yao wakayaamua, na wao wakatiiwa,
Hata ikiwa kuua, na bado wakachiwa,
Ya nchi yanatushinda, twafata ya ulimwengu?

Wasafi tukishakua, nchi ikawa yang'aa,
Pasiwe harufu mbaya, katika yetu mitaa,
Watatukimbilia, hata tusiowajua,
Ya nchi yanatushinda, twafata ya ulimwengu?

Kipaumbele twavia, mambo yanajiendea,
Hata yapaswayo kuwa, kwa sasa yanatukataa,
Kila ukiangalia, maongozi yafifia,
Ya nchi yanatushinda, twafata ya ulimwengu?

Mlima umepotea, vichuguu vimejaa,
Kwa mchwa sasa valiwa, hakuna linalokuwa,
Watu ni kujisifia, na mali kujilimbikia,
Ya nchi yanatushinda, twafata ya ulimwengu?

Kalima nimeitoa, na samahani natoa,
Pale nilipokosea, naomba kusamehewa,
Mimi mja nisojua, ajuaye ni Allaa,
Ya nchi yanatushinda, twafata ya ulimwengu?

Mimi mja nisojua, ajuaye ni Allaa,
Mkubwa aliyekuwa, na juu ameulia,
Apaswaye abudiwa, wengine shiriki huwa,
Mimi mja nisojua, ajuaye ni Allaa,
Ya nchi yanatushinda, twafata ya ulimwengu?

Februari 29, 2012.
Dar es Salaam. Tanzania.
East Africa.

No comments: