Friday, February 3, 2012

Wagonjwa siyo ishuu

Kwa niliyowaelewa, ijapo hawakuongea,
Wana mengi watakiwa, wao kuyazungumzia,
Ila si Watanzania, leo wanaougua,
Wagonjwa siyo ishuu, wabunge watuambia ?

Ila si Watanzania, leo wanaougua,
Au roho wanaoachia, kufatia kugomewa,
Kwa mgomo unaoenea, na kila siku kuua,
Wafao sio ishuu, wabunge watuambia?

Posho yao ingekuwa, mara moja wapigania,
Ila ya wasahauliwa, serikali yaachiwa,
Maana sijaijua, nchi na wabunge kuwa!
Wagonjwa siyo ishuu, wabunge watuambia ?

Mimi ninavyoelewa, wananchi kutetea,
Kwa hali na mali pia, maafa kuja tokea,
Wafao sio ishuu, wabunge watuambia?
Salama wawe raia, wa nchi yetu Tanzania,
Wagonjwa siyo ishuu, wabunge watuambia ?

Upinzani walizua, wenye nchi kukataa,
Hakuna kuzungumzia, uzito yasiyokuwa,
Maana kazi wajua, ni wakubwa kutetea,
Wafao sio ishuu, wabunge watuambia?

Uwajibikaji nazaa, nchi ilivyopotea,
Na Mwenyezi hujalia, zikazaana balaa,
Nuksi na mikosi pia, kwa laana zinazojaa,
Wagonjwa siyo ishuu, wabunge watuambia ?

Mola tunakuangukia, watu kutusaidia,
Hoi juu walokuwa, majukumu wayakimbia,
Ndiwe uliyebakia, nani wa kutegemea?
Wafao sio ishuu, wabunge watuambia?

No comments: