Monday, February 20, 2012

Mchaga kuwa Masai

Mwinyi ulichonambia, hakika nafikiria,
Kwanza nilikatalia, sasa nakukubalia,
Baada ya kuambiwa, miye nisiyoyajua,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Inaweza kutokea, Mchaga akichagua,
Uamuzi ulokuwa, itihari kutumia,
Maslahi akijua, asili huikataa,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Waafrika nawajua, kuwasoma naelewa,
Kabila sasa lanywea, faida waangalia,
Na mwana kulikimbia, kawaida imekua,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Hii yetu Tanzania, kiongozi hutokuwa,
Kabila ukitokea, ukubwa lililojaliw,
Wadogo wanatakiwa, nchi ndogo kudumaa,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Wakubwa wanahofiwa, ukabila watatia,
Ila hawajafikiria, atakachopigania,
Pengine mawazo kuwa, ndiyo yenye kutufaa,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Udogo unatakiwa, hata uwazir pia,
Haijawahi tokea, kabila kubwa kutoa,
Waziri mkuu kuwa, Usukuma kazaliwa,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Haijawahi tokea, Mchaga rais kuwa,
Kwani atuhumiwa, Hazina ataibomoa,
Na wengine kuwaibia, pasiwe kitu chabakia,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Mhaya wanamkimbia, ukabila aujua,
Nchi ukimuachia, Kihaya wataongea,
Mashaka mmejionea, komedi yakitokea,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Myamwezi atumiwa, mizigo kutubebea,
Ukubwa hataupewa, Mmakonde huachiwa,
Hii viza filosofia, nguvu yake yapungua,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Wakati umewadia, vipaji kuangalia,
Mambo walojifanyia, hadi juu kuingia,
Uchumi wanaojua, sio wanaotegeme,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Kabila dogo hupwaya, sayansi yatwambia,
Jamii iliyokuwa, mtu inamwangalia,
Mawazo yanaishia, mipaka ilipokuwa,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Kabila kubwa likiwa, fikra kubwa hukua,
Mbali wakajionea, wadogo wasiojua,
Ndipo tulipofikia, na bado hatujajua,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Ila inaelekea, mwiko imeshakuwa,
Mkubwa kufikiria, uongozi kuutwaa,
Hivi tutajaendelea, mtaji huu ukiwa?
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Ndio maana wavua, makabila walokuwa,
Mchaga akachagua, Umasai kuingia,
Watu wasipomujua, mwisho watamchagua,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Unafiki umekua, na sisi tunaulea,
Hekima kuitumia, huru kweli watu kuwa,
Asili kuiringia, na nchi kutumikia,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Na kama yetu mikoa, waziri mkuu akiwa,
Na wabunge kuridhia, wa mkoa kuchagua,
Bunge wakajiundia, na mawaziri wakawa,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Ushauri nautoa, kamati umma kwachia,
Marais kuteua, kisha kura kupigiwa,
Wagombe waliokuwa, katika kila mkoa,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Hadi kila chama kuwa, na mmoja chabakia,
Hao kilingeni kwingia, mshindi tukamjua,
Kamati zikichagua, zaweza kupendelea,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Na zaweza nunuliwa, na hela waliokuwa,
Mlaji kumchagua, nchi akatuharia,
Zaidi ya ilivvyokuwa, tubakie tunalia,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

Uhuni utapungua, na ukweli kuridhiwa,
Mwanaharamu kwishiwa, ujanja kutotumia,
Kombe likafunuliwa, uwazi ukaenea,
Mchaga kuwa Masai, inaweza kutokea!

No comments: