Monday, February 20, 2012

Wa juu wakiwa wezi

ASILI ilivyokuwa, na huwezi kuzuia,
Juu wezi wakikaa, chini nao hufatia,
Uoza ukaenea, kila mahali ukawa,
Wa juu wakiwa wezi, wa chini wa'che kuiba?

Nchi zataka ulua, watu wasio tamaa,
Wajuao kutulia, na mambo kufatia,
Sio wanaosinzia, na wengine kuachia,
Wa juu wakiwa wezi, wa chini wa'che kuiba?

Hao wanaoachiwa, hugeukia ubaya,
Mengi wakajifanyia, nchi isiyoyafaa,
Na dhuluma kuitia, kila katika hatua,
Wa juu wakiwa wezi, wa chini wa'che kuiba?

Ndipo tulipofikia, na dunia inajua,
Yaona twaikosea, utawala tunapwaya,
Mambo tunayaachia, yenyewe yajiendea,
Wa juu wakiwa wezi, wa chini wa'che kuiba?

Na wengine washania, ushirika tumekua,
Na wahuni watuvaa, na mfukoni kututia,
Na kila tukiamua, ni wao yanayowafaa,
Wa juu wakiwa wezi, wa chini wa'che kuiba?

Kila mwana ajisemea, hilo analolijua,
Ukweli hatujajua, maana hatujaambiwa,
Uongo tumezoea, ukweli tunauchelea ?
Wa juu wakiwa wezi, wa chini wa'che kuiba?

Kila wizara yalia, na idara nazo pia,
Salama imepotea, kwa watu na mali pia,
Ulinzi ajizi yawa, kubaya twaelekea,
Wa juu wakiwa wezi, wa chini wa'che kuiba?

Nchi sasa yaibiwa, kushoto pia kulia,
Na ndani wametulia, haya wanaojifanyia,
Ulemavu twajitia, na upofu nao pia,
Wa juu wakiwa wezi, wa chini wa'che kuiba?

Amkeni mwasinzia, kuwa macho mwatakiwa,
Arijojo Tanzania, ndege sasa inapaa,
Mlima kuuvamia, ni rahisi itakuwa,
Wa juu wakiwa wezi, wa chini wa'che kuiba?

Hatari inatujia, kuamka tunatakiwa,
Rubani kwenda mshtua, apime wanaomsaidia,
Yaelekea jamaa, hawajui yalokuwa,
Wa juu wakiwa wezi, wa chini wa'che kuiba?

Ushahidi nimetoa, nami kuja shuhudiwa,
Niliona, nikajua, na wengine kuwaambia,
Hakuna alonisikia, hadi shari kutokea,
Wa juu wakiwa wezi, wa chini wa'che kuiba?

Na kizazi kitajua, mkweli aliyekuwa,
Iandike historia,waliofanza sanaa,
Wakajitia kujua, hata wale wasojua,
Wa juu wakiwa wezi, wa chini wa'che kuiba?

Yafaa kumgeukia, Mola kutuhurumia,
Majaribu katutia, tunashindwa kujitoa,
Kila mtu aumia, na sifa zinapungua,
Wa juu wakiwa wezi, wa chini wa'che kuiba?

Februari 23, 2012.
Pangani. Tanzania.

No comments: