Monday, February 20, 2012

Huvuna tusikopanda

Nia wasiojaliwa, yao huyakusudia,
Nchi wataibomoa, wao wapate kukua,
Watu wanatushangaa
Kuvuna tusikopanda, wasiwasi ni wa nini?
Na wajinga wamejaa.

Nchi hujichuuzia, yao yapate kuwa,
Dalali wakanunua, watumwa wawe raia,
Wauza nchi kuvaa
Kuvuna tusikopanda, wasiwasi ni wa nini?
Na wajinga wamejaa.

Ugenini huingia, ya kwao akachukua,
Nyumbani kuyatumia, yake akajitupia,
Asili wasiojua
Kuvuna tusikopanda, wasiwasi ni wa nini?
Na wajinga wamejaa.

Kweli ataikataa, uongo akapokea,
Na kisha akaamua, kwalo asilolijua,
Uongo kuuvumbua
Kuvuna tusikopanda, wasiwasi ni wa nini?
Na wajinga wamejaa.

Njaa huwatangulia, upofu kuwaingia,
Mfukoni wakatiwa, kama chenji ilokuwa,
Viongozi wenye njaa
Kuvuna tusikopanda, wasiwasi ni wa nini?
Na wajinga wamejaa.

Fedha wanaokimbilia, na Mungu wao ikawa,
Akili zinapoishia, nani wa kuwajalia,
Chama kikitekwa nyara
Kuvuna tusikopanda, wasiwasi ni wa nini?
Na wajinga wamejaa.

Hufanzwa nao bidhaa, bei wakajawekewa,
Kisha wakanunuliwa, na wakwasi kutumiwa,
Wakubwa wakinunuliwa
Kuvuna tusikopanda, wasiwasi ni wa nini?
Na wajinga wamejaa.

Aibu huwakimbia, haki wakachuuzia,
Na nyingi anayetoa, yeye akainunua,
Haki zinaponadiwa
Kuvuna tusikopanda, wasiwasi ni wa nini?
Na wajinga wamejaa.

Ndipo tulipofikia, Kariakoo Tanzania,
Wazee waumbuliwa, hawana pa kukimbilia,
Wanyonge kuwararua
Kuvuna tusikopanda, wasiwasi ni wa nini?
Na wajinga wamejaa.

Wazima waliokuwa, hufanywa nao vichaa,
Mchana kuhadaiwa, na juu lawaka jua,
Wajinga kuwahadaa
Kuvuna tusikopanda, wasiwasi ni wa nini?
Na wajinga wamejaa.

Mbeleko walofungiwa, huzidi kuning'inia,
Mchango wasiotoa, ila tu ni kupokea,
Wabebwao kuwalea
Kuvuna tusikopanda, wasiwasi ni wa nini?
Na wajinga wamejaa.

Nchi ikadidima, mamluki kuingia,
Utapeli ukakua, na mali zikapota,
Mamluki kutumia
Kuvuna tusikopanda, wasiwasi ni wa nini?
Na wajinga wamejaa.

Na wasipodhibitiwa, maafa yatatokea,
Nchi kuparaganyikiwa, na watu kuchanganyikiwa,
Demokrasia kuua
Kuvuna tusikopanda, wasiwasi ni wa nini?
Na wajinga wamejaa.

No comments: