Friday, February 3, 2012

Mola anayemwongoza

Mola anayempenda, atamuonyesha njia,
Hawezi katu kupinda, njiani akapotea,
Safari ya mijikenda, humtosha siku moya,
Mola anayemwongoza, sikuzote yuko sawa!

Mola aliyemktaa, na shetani kumvaa,
Hata nyeupe ikiwa, njia anamopitia,
Hatoacha kupotea, hata akiulizia,
Mola asiyemwongoza, daima yu na shetani !

Mola anayemlilia, daima humsikia,
Ushauri kumgeya, mbele akaendelea,
Hakutani na balaa, kadhalika na vichaa,
Mola anayemwongoza, sikuzote yuko sawa!

Ukubwa hukimbilia, na juu kujinyanyua,
Mafuu akadhana, wafuasi wamekua,
La mtu hatosikia, hata la kumuokoa,
Mola asiyemwongoza, daima yu na shetani !

Hujua asiyejua, Mola akimsimamia,
Ndoto atazing'amua, yafaayo kuamua,
Wazushi hatosikia, kwa lao akaamua,
Mola anayemwongoza, sikuzote yuko sawa!

Ya chini hatoyajua, wala hawezi sikia,
Uongo ataambiwa, na kweli akadhania,
Huamini asifiwa, kumbe wote wamzomea,
Mola asiyemwongoza, daima yu na shetani !

Wanafiki walokuwa, daima huumbuliwa,
Walio safi kujaa, na maovu kuambaa,
Adhana huisikia, Bwana akamwitikia,
Mola anayemwongoza, sikuzote yuko sawa!

Wakware atachagua, wamharibu kwa madoa,
Jina hujichafulia, asiweze kulifua,
Mwishowe kuwa kinyaa, marashi akidhania,
Mola asiyemwongoza, daima yu na shetani !

Huambaa wakumfaa, akawabeba adawa,
Kaburi hujichimbia, bila ya yeye kujua,
Akija kushtukia, aona anafukiwa,
Mola asiyemwongoza, daima yu na shetani !

Hujaliwa majaliwa, akawapata radhia,
Hata asiowajua, moyoni wakamjaa,
Salama kuhifadhiwa, dhara kutomtokea,
Mola anayemwongoza, sikuzote yuko sawa!

Upuuzi huusikia, hekima akadhania,
Ujinga huuchukua, busara akiijua,
Uongo huuridhia, ukweli akiaminia,
Mola asiyemwongoza, daima yu na shetani !

Macho atafunguliwa, hata anaposinzia,
Haki na kweli kujua, pembeni kutopitia,
Iliyonyooka njia, iwe aliyochagua,
Mola anayemwongoza, sikuzote yuko sawa!

Pasafi huwa akaa, Malaika kumjia,
Akichoka humpepea, ikiwa asoma dua,
Wanaomkurubia, Mola keshawaridhia,
Mola anayemwongoza, sikuzote yuko sawa!

Shetani hukaribia, uchafu ulivyojaa,
Na machafu kuingia, bila wa kuyazuia,
Na uoza hunukia, vyote vikawa kinyaa,
Mola asiyemwongoza, daima yu na shetani !

Februari 5, 2012,
Dar es Salaam.

No comments: