Monday, February 20, 2012

Mtumba au kaniki, ipi ina afadhali?

Huko tulikotokea, kaniki tuliivaa,
Mzungu hakutujua, wala kutusaidia,
Uhuru kujipatia, mitumba tumerudia,
Mtumba au kaniki, ipi ina afadhali?

Yupi kutamba afaa, kaniki na hiyo keyaa,
Majira yanaishia, achakaa Mtanzania,
Kila alichobarikiwa, nuksi sasa imekua,
Mtumba au kaniki, ipi ina afadhali?

Mtumba au kaniki, ipi ina afadhali?
Mapumba tunajilia, na urembo wapungua,
Lishe tumashaishiwa, na uzuri nao pia?
Mtumba au kaniki, ipi ina afadhali?

Wazee wametangulia, nchi wametwachia,
Siku wakifufuliwa, hawatoacha shangaa,
Hivi ndivyo imekua, nani anawaumbua:
Mtumba au kaniki, ipi ina afadhali?

Ghorofani walokaa, haya wanayasikia,
Kuamini wakataa, wasema tunaendelea,
Na takwimu wazitoa, matope kupakazia,
Mtumba au kaniki, ipi ina afadhali?

Watu kweli waumia, kimya kimya walia,
Waamini ni udhia, vingine kuwaambia,
Na siku ikitokea, pengine kusaidiwa:
Mtumba au kaniki, ipi ina afadhali?

Waishi kwa kutumainia, milo mitatu ikawa,
Kwa sasa wapigania, mmoja tu kujipatia,
Na sisi twajisifia,na juu kujinyanyua,
Mtumba au kaniki, ipi ina afadhali?

Wanaosherehekea, msiba watuitia,
Na siku ikifikiya, haya mtayatambua,
Ghaibu ninayoijua, ukweli inshanambia:
Mtumba au kaniki, ipi ina afadhali?

Hakuna cha kufunua, na kufunika ruia,
Uchi nchi kubakia, kwa kilio cha kuliwa,
Mwalia huku mwaliwa, ni ijayo historia:
Mtumba au kaniki, ipi ina afadhali?

No comments: