Tuesday, February 28, 2012

Miradi ya kuibia raia

WAMEIZUSHA tabia, wananchi kuwaibia,
Wanatakiwa kutoa, hata wasichojaliwa,
Hii shari inakuwa, zahama naihofia:
Miradi ya kuibia, raia mnayozua,
Viongozi nawaonya
Mwatakiwa angalia
Msije zua balaa!

Wema watashingilia, kauli ninayotoa,
Maana wanatambua, mbele yanayowangojea,
Dhuluma waichelea, na haramu kukimbia:
Miradi ya kuibia, raia mnayozua,
Viongozi nawaonya
Mwatakiwa angalia
Msije zua balaa!

Ila wabaya najua, tena sana wachukia,
Makaa ya moto haya, sasa wanayojilia,
Masikini wanajua, ni uhondo uliokuwa:
Miradi ya kuibia, raia mnayozua,
Viongozi nawaonya
Mwatakiwa angalia
Msije zua balaa!

Ila siwezi chelewa, ukweli wangu kutoa,
Sitaki kuwahadaa, uongozi sintogombea,
Kweli tupu ninatoa, na Mola namwangukia:
Miradi ya kuibia, raia mnayozua,
Viongozi nawaonya
Mwatakiwa angalia
Msije zua balaa!

Unafiki umejaa, kwenye zetu manispaa,
Ukweli tunaujua, ila tunauambaa,
Tunaoneana haya, wabaya kuwafichua,
Miradi ya kuibia, raia mnayozua,
Viongozi nawaonya
Mwatakiwa angalia
Msije zua balaa!

Manasara nawajua, haya amri zakataa,
Hata dini wasokuwa, maovu wanajua,
Vipi mliochaguliwa, na walioteuliwa?
Miradi ya kuibia, raia mnayozua,
Viongozi nawaonya
Mwatakiwa angalia
Msije zua balaa!

Vipi mliochaguliwa, na walioteuliwa?
Mnataka kunambia, dhambi hamjaijua,
Wakazi mwawafanyia, hali vipofu mkiwa?
Miradi ya kuibia, raia mnayozua,
Viongozi nawaonya
Mwatakiwa angalia
Msije zua balaa!

Wenyewe mnajiua, na kizazi kujavia,
Kiwe kilicholaaniwa, kwa haramu kutumia,
Hadi wajukuu kuwa, maaluni na vichaa:
Miradi ya kuibia, raia mnayozua,
Viongozi nawaonya
Mwatakiwa angalia
Msije zua balaa!

Mola mkimgeukia, thuma mtasamehewa,
Kwake mkisharejea, miji bora itakuwa,
Ukaondoa udhia, kwa wageni na raia:
Miradi ya kuibia, raia mnayozua,
Viongozi nawaonya
Mwatakiwa angalia
Msije zua balaa!



Februari 28, 2012.
Dar es Salaam. Tanzania.
East Africa.

No comments: