Monday, February 20, 2012

Nchi inaendelea au inarudi nyuma ?

(Tahadhari unayejua.)

Hata roho ndogondogo nazo zinatupotea !
Nashindwa osha mgongo, kwa maji kujimiminia,
Ninaukataa uongo, eti tunaendelea:
Hata roho ndogondogo, nazo zinatupotea,
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Pengine twaendelea, kwa rivasi kutumia,
Ni gia tusojua, miti mbele yasogea,
Na sisi tukadhania, ndio inayotembea:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Bafuni nikingia, bethitabu lachakaa,
Maji halijayajua, miongo imeshakua,
Na kisha wanambia, eti tunaendelea:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Kwingine siwashi taa, na jiko nalifungia,
Umeme nikichezea, mwisho nitafilisiwa,
Mapambo yamebakia, wanambia najongea:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Vinywaji navikimbia, wana wasife kwa njaa,
Nikithubutu kutwaa, shilingi itaniumbua,
Hata kiu kuitoa, sasa ni kubwa kadhia:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Chakula kimepungua, twala kwa kupimia,
Kidogo ukichelewa, mgeni aje ni njaa,
Na kuficha haijawa, imani yalikataa,
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Sinema kuangalia, ni zile zilizochakaa,
Mpya ukiinua, bajeti itakataa,
Starehe zapungua, imebakia kuzaa,
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

TV kuinunua, nyumbani utawaua,
Na shule wakatolewa, ada haitotimia,
Wenyewe si wa kuchelewa, mkono mbele watoa:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Gazeti kulinunua, kazi kubwa imekua,
Kitabu hujanunua, huwezi kuulizia,
BP watakutia, bure bure kujifia:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!


Michezo wanaingia, heri waliojaliwa,
Hata bure kilokuwa, wenyenacho wazuia,
Watuhasi tukijua, na kusema twaendelea:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Hata chai kujinywea, ni anasa inakuwa,
Sukari ukinunua, mlo waweza kimbia,
Wamepwaya mashujaa, mfukoni wametiwa:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Kahawa naihofia, bei nayo impeaa,
Kwani ukitembezewa, nawe kutembeza huwa,
Kila nikihesabia, nahofu kujiumbua:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!


Kijiwe nakikimbia, kuuogopa udhia,
Wakajua nimeishiwa, nashindwa hata kahawa,
Hii ndiyo Tanzania, nchi iliyojaliwa:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Neema imepotea, mitumba tunaivaa,
Nayo si kuchagua, kusakura yatakiwa,
Na jioni kuvizia, rahisi zinapokua:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Ukienda kutibiwa, kiwewe utaingia,
Wengine wanaamua, kimya kimya kujifia,
Kuliko kuumbuliwa, na huruma wasokuwa:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Shule na vyuo pia, na yao yakifikia,
Hutamani kukimbia, nchi ukawaachia,
Na wathubutu kutwambia, si hapa ni huko Ulaya:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Hapa ni ya kuchelewa, lakini yanatujia,
Zaidi ya ilivyokuwa, na hakuna kujiandaa,
Ubabe tunajitia, mkojo tutaachia:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Mipango mnazubaa, hamtaki jiandaa,
Siku mnaingojea, na yake msiyojua,
Uongozi haujawa, sivyo unavyotakiwa:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Uongozi watakiwa, yajayo kuyatambua,
Na mikakati kutia, kwa nchi kuinasua,
Afadhali kuja kua, sio tu twajikalia:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!

Kombora la nyuklia, kiuchumi latujia,
Nasi twaangalia, na wengine kuchekea,
Bila maji kunyolewa, ndivyo hivyo itakuwa:
Eti ni wanathubutu,
Eti wameshajaribu
Eti wanasonga mbele
Kweli kinyume cha hayo!


Februari 21, 2012
Dar es Salaam. Tanzania.

No comments: